Categories
Habari Siasa

Wabunge Wataka Mbunge Condester Sichwale Aliyetolewa Nje Na Spika Ndugai Kwa Madai Ya Mavazi Yasiyo Ya Kimaadili Aombwe Radhi

Sakata la kutolewa nje kwa mbunge wa Momba, Condester Sichwale (CCM) kuhusu mavazi, limeibuka tena leo jioni katika kikao cha Bunge baada ya wabunge wanawake kutaka aombwe radhi na aliyetoa hoja.

Hata hivyo mbunge Hussein Amar amesema hawezi kuomba radhi kwa sababu alichosema alikuwa sahihi kwakuwa mavazi aliyovaa mbunge mwenzake hayakuwa na staha ndiyo maana Spika wa Bunge Job Ndugai aliridhia hoja aliyoitoa yeye (Amar).

Katika kikao cha leo jioni wabunge Jacqueline Ngonyani na Stella Manyanya waliomba mwongozo wa Spika kwa madai mbunge aliyetolewa nje alionewa.

Mapema leo Sichwale alitolewa nje kwa amri ya Spika baada ya Amar kuomba mwongozo kwa kutumia kanuni 170 kuhusu mavazi ya staha.

Ngonyani amesema kilichotokea ni kwamba mbunge huyo alionewa kwani alikuwa na vazi la staha ambalo halikuwa na shida lakini akasema huenda Spika hakuona.

“Mimi ni mjumbe wa Baraza Kuu la wanawake wa CCM, ninapoona kuna uonevu lazima niseme na hili sikiungi mkono huyu mwanamke mwenzetu ameonewa,”amesema Ngonyani.

Mbunge huyo amesisitiza kuwa uonevu wa namna hiyo haupaswi kuvumiliwa kwakuwa umemdhalilisha mbunge huyo na wapiga kura wake jimboni.

Kwa upande wake Manyanya amesema tangu asubuhi alikuwa anafuatilia kwenye mitandao na amebaini kuwa Sichwale hakuwa na vazi baya.

Hata hivyo Manyanya amesema haiwezekani wabunge vijana wavae mavazi kama wanayovaa wabunge wanawake watu wazima.

Amesema katika siku za karibuni limeibuka suala la kutoa lugha za kuwadhalilisha wabunge wanawake ndani ya ukumbi ambako wakati mwingine hutamkwa kiungo cha mwanamke halafu wengine wanafurahi.

Naibu Spika Dkt. Tulia Akson amesema atatoa mwongozo baada ya kufuatilia jambo hilo.