Categories
Habari Siasa

Mgogoro NCCR-Mageuzi: Msajili abariki Mbatia kusimamishwa

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini imebariki kusimamishwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia na Sekretarieti yake yote, kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho hadi uamuzi huo utakapoamuliwa vinginevyo.

Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza amesema uamuzi wa Kikao cha Halmashauria ya chama hicho kilichofanyika Mei 21 mwaka huu, ulikuwa halali.

Hii ni baada ya ofisi yake kupokea barua ya kusimamishwa kwa Mbatia na Makamu wake kwa mujibu wa sheria.

Mbatia alisimamishwa sambamba na makamu wake Bi Angelina Mtahiwa hivi karibuni.

Nyahoza amesema kwa mamlaka ya ofisi hiyo, inamtaka Mbatia kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho hadi uamuzi huo utakapotenguliwa na chama.

“Tumepokea barua ya chama juu ya maamuzi yaliyofanyika, hivyo hawatakiwi kujihusisha na mambo ya chama,” amesema.

” Kama hawataridhika, basi watafute haki mahakamani,” amesema.

Mei 21 mwaka huu, Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi ilimsimamisha Mbatia na makamu Mwenyekiti Bara kutojihusisha na shughuli zozote za chama hadi mkutano mkuu utakapoitishwa ili wajieleze kuhusiana na tuhuma zinazowakabili.