Categories
Habari Siasa

Mama @SuluhuSamia Ajibu Ombi la @zittokabwe kumsihi Rais Asaidie Kuachiwa kwa Mbowe

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amevunja ukimya kuhusu kinachomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe akisema kuwa demokrasia ni kuheshimu sheria.

Akizungumza leo Jumanne Desemba 15, 2021 wakati akifungua mkutano wa wadau kujadili demokrasia ya vyama vingi, Rais Samia amesema ni muhimu kuzingatia sheria za nchi.

Mkuu huyo wa nchi ameyasema hayo akijibu ombi la Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) Zitto Kabwe aliyemuomba kusaida kuachiwa kwa Mbowe ambaye pamoja na wenzake watatu wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021 yenye mashtaka sita yakiwemo ya kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi, inayoendelea katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Rais Samia amesema, “Nataka nijibu lile ombi la mwanangu, iko hivi demokrasia ni kuheshimu sheria, unapoheshimu sheria ndipo demokrasia inapokua, lakini pia ndipo inapoleta heshima.

“Heshima ya mtu inakuja unapoheshimu sheria za nchi, unapovunja sheria za nchi heshima yako haitaheshimiwa, Serikali haitakuheshimu lakini lazima ujue kwamba unapotumia uhuru wako mwisho wa uhuru wako inaanza heshima ya mtu mwingine,”.

Ameendelea,’’Isingekuwa uvunjifu wa sheria leo isingemlazimu Zitto kuomba hapa kwamba yule mwenzetu muachie lakini unapovunja sheria unajivunjia heshima

“Naomba tufanye kazi kwa kuheshimu sheria, waswahili wanasema mtaka nyingi nasaba hupata mingi misiba, ingawa kusameheana nako kupo,” amesema Samia.