Categories
Habari Siasa

“Mama Samia Amepotoshwa Au Ameamua Kusema Uongo Katika Ufafanuzi Wake Kuhusu Kesi Ya Mbowe” – Chadema

Chama cha upinzani nchini Tanzania Chadema, kimesema rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan “aidha amepotoshwa au ameamua kusema uongo” katika baadhi ya mambo ambayo ameyatolea ufafanuzi katika mahojiano yake maalumu aliyofanya na BBC.

Kauli hiyo, imetolewa hii leo na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika pindi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mnyika, amepinga baadhi ya hoja zilizotolewa a rais Samia ikiwemo zile zinazodai kwamba, Mbowe kwa muda mrefu alikuwa nje ya nchi baada ya kujua ana kesi inayomkabili, hivyo kusema, “hakuna wakati ambao kiongozi huyo ametoroka nchi au amekuwa nje ya nchi kinyume cha sheria.”

Mnyika ameongeza kusema kuwa, wakati ukifika, “chama kitatoa vielelezo vitakavyoonyesha uhalali wa safari hizo.”

Hata hivyo, rais Samia alipoulizwa iwapo kesi hiyo ya Mbowe ni ya kisiasa, alikataa kulitolea ufafanuzi wa kina kwa kusema kuwa, tayari kesi hiyo iko mahakamani, hivyo ni vyema kuachia mahakama kufanya kazi yake.

Lakini tayari Chadema inamlaumu rais Samia kwa madai kwamba ameingilia uhuru wa mahakama, na kusema, wameongeza na jopo la mawakili wao ili kuona ni hatua gani wanaweza kuchukua.

Aidha miongoni mwa mambo mengine ambayo Chama hicho kimeyajibu ni pamoja na kauli ya rais aliposema kuna tofauti kati ya demokrasia ya kisiasa na fujo za kisiasa, hivyo kuashiria kwamba, baadhi ya maandamano yanayoitishwa na vyama vya kisiasa kama fujo za kiasa.

Hata hivyo, kauli hii inaonekana kuwa mwiba kwa chama hicho cha upinzani ambapo Mnyika amesema kupiga marufuku mikutano hiyo ya hadhara ni kinyume cha katiba ya nchi na sheria za vyama vya kisiasa.

Chadema pia imedai kwamba rais Samia amepotosha umma pale aliposema kwamba, wananchi wamekubali tozo za simu, ila kiwango cha tozo ndio hawajakikubali.

Nchini Tanzania kumekuwa na maoni tofauti baada ya BBC kufanya mahojiano na rais Samia ambayo yamegusia nyanja mbalimbali ikiwemo masuala ya demokrasia, uhuru wa vyombo vya habari pamoja na masuala mengine kadhaa.

Source: BBC Swahili