Categories
Habari Siasa

CCM Waanza Kutiana Vidole Machoni: Bulembo Amuwakia Polepole, Adai Bashiru Alikuwa mwana-CUF, Amponda Prof Kabudi Akimtuhumu Kuharibu Mahusiano Kimataifa

Mwenyekiti mstaafu wa jumuiya ya wazazi ya CCM, Abdallah Bulembo amemtaka mbunge wa kuteuliwa, Humphrey Polepole amwache Rais Samia Suluhu Hassan atekeleze majukumu yake.

Ametoa kauli hiyo leo Jumapili Desemba 12,2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari akimjibu Polepole kuhusu lawama alizotoa dhidi ya Samia ambaye ni mwenyekiti wa CCM.

Bulembo amemuomba makamu mwenyekiti wa chama hicho bara, Philip Mangula kumuhoji Polepole kama alivyowahoji makatibu wakuu wa zamani, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba ambao sauti zao zilivuja wakikosoa viongozi na mwenendo wa chama hicho tawala, akitaka Polepole naye aitwe kamati ya maadili.

Huku akisisitiza kuwa anakemea suala hilo kama mwanachama wa kawaida na hajatumwa na mtu amesema, “kama Polepole anataka kutoka atoke atuachie CCM maana ana wenzake wanaomshawishi kuanzisha chama chao, asitapetape na kuongea mambo ambayo hayaeleweki.”

“Hawa kina Polepole waliojificha hawatusumbui ndani ya CCM kwa mujibu wa kanuni na katiba ya chama kama mwanachama anaenda tofauti kuna onyo, kufungiwa au kufukuzwa uanachama.”

Bulembo amesema anamfahamu Polepole tangu mwaka 2012 alipoteuliwa na rais mstaafu Jakaya Kikwete kuwa mjumbe wa iliyokuwa tume ya mabadiliko ya katiba.

“Siyo kwamba ndani ya CCM tulifurahia uteuzi wake wa ukatibu mwenezi Taifa bali tuliheshimu mamlaka ya aliyekuwa mwenyekiti Taifa hayati John Magufuli bali. Hamjali Samia na kimsingi hawezi kumpangia rais cha kufanya, yeye ni nani,”amesema Bulembo