Categories
Habari Sayansi

Kukabiliana na Janga La Korona Tanzania Na Kukidhi Matakwa Ya IMF: Serikali ya Mama Samia Yaagiza Uvaaji Barakoa Kwenye Mikusanyiko

Serikali ya Tanzania imeagiza wananchi kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa corona kwa kuvaa barakoa sehemu zenye mikusanyiko, ili kujikinga na wimbi la tatu lililoibuka katika mataifa mbalimbali.

Wakuu wa mikoa na wilaya wameagizwa kuhakikisha wanatimiza agizo hilo kwa kuzishirikisha kamati za afya ya msingi na kwamba watapimwa kulingana na utendaji wao.

Pamoja na hatua mbalimbali ambazo Tanzania imeanza kuchukua, Shirika la Fedha Duniani (IMF) limethibitisha kwamba litaipatia Tanzania mkopo wa dharura wa takribani dola milioni 574, itakapokamilisha mambo muhimu, ikiwemo utoaji wa takwimu kuhusu maambukizi ya virusi vya corona.

Akizungumza Jumamosi Juni 12 , Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima aliagiza pia wananchi kuchukua tahadhari kwa kurejesha utaratibu wa kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka na matumizi ya vitakasa mikono ‘sanitizer’.

Alisema Tanzania inazungukwa na nchi nyingi Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla na kwamba inapokea wageni wengi kutoka nchi mbalimbali.

“Kamati iliyoundwa na Rais ilisema tupo salama, ila Mei 17 mwaka huu Brazil, India na nchi nyingine zilikuwa zinapigwa na wimbi la tatu la ugonjwa huu. Kwa hiyo wakasema hata sisi lazima tujitahadharishe na tujizatiti ili kuhakikisha wimbi hili haliingii kwetu, hivyo tusiliruhusu,” alisema Dk Gwajima.

Dk Gwajima alisema utaratibu wa kuvaa barakoa unapuuzwa, hali ambayo ni hatari, kwani Tanzania imezungukwa na nchi ambazo tayari zinapigwa na wimbo la tatu, ikiwemo Uganda na Congo.

Alisema Wizara pamoja na wataalamu katika viwanja vya ndege, mipakani pamoja na wananchi wanaotoka na kuingia wanaendelea kuchukua tahadhari.

“Tunashuhudia watu wamesongamana na hawavai barakoa, sasa wanatupatia kazi sisi mawaziri wa afya, viongozi wa Serikali kupambana na hali hii, sijasema ukienda shambani kulima uvae barakoa kwa kuwa huwezi kuvaa saa 24, lakini kuna mazingira ukishafika unaona kabisa hapa pana msongamano hewa haizunguki vizuri vaa,” alisema.

Alisema Serikali imeshatoa miongozo, kilichobaki ni utekelezaji, wananchi wachukue tahadhari.

Dk Gwajima alisema kazi ya kuelimisha wananchi inatakiwa ifanyike kuanzia ngazi za chini za wakuu wa wilaya kwa wakuu wa mikoa si kazi ya waziri peke yake au katibu mkuu.

Alisema kuna ulegevu katika kutoa elimu kwa wananchi, huku akisema mapema wiki hii Wizara imepanga kuitisha kikao pamoja na wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.

“Kule waliko wana kamati zao zinazoitwa kamati za afya ya msingi, ambazo mwenyekiti wake ni mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya, wao wanatakiwa waite sekta zote zilizopo pale iwe ni elimu, kilimo, maji wajadili na kupeana kazi juu ya miongozo ambayo Wizara tumekuwa tukiitoa ili kufikisha elimu kwa wananchi,” alisema Dk Gwajima.

Alisema tatizo kubwa ni baadhi ya wananchi kutofikishiwa taarifa kuhusu kuchukua tahadhari.

“Hatuwezi kuwafikia wote, lazima tuwatumie viongozi hawa na kadri tunavyoenda tutasainishana nao mikataba ili kuwapima kulingana na haya, mkoa gani unafanya vizuri, tunaita ‘score card’ ambaye hajafanya vizuri tunadili na mamlaka yake ya kuwajibika,” alisema.

Chanzo: Mwananchi