Categories
Maoni Siasa

Maoni Ya Mdau: Tatizo Sio Katiba Mpya Bali Kutotii Sheria Zilizomo Kwenye Katiba Iliyopo. Kama Sheria Zilizo Kwenye Katiba Ya Sasa Zapuuzwa, Miujiza Gani Itafanya Zilizomo Kwenye Katiba Mpya Ziheshimiwe?

Maoni ya mdau mmoja huko Jamii Forums

Mjadala wa madai ya Katiba mpya unaendelea kushika hatamu. Baadhi yetu wanadai kuwa nchi inahitaji Katiba mpya, wanatoa sababu zao. Madai yao ni ya kuheshimiwa kwa sababu ni haki yao lakini ni yenye kustahili kusahihishwa kwa sababu si ya kweli. Ni uongo!

Kwa ajili ya kumbukumbu, nimekusudia kusahihisha madai ya Katiba mpya kama yanavyotolewa. Kimsingi, tatizo la Tanzania kwa wakati huu sio Katiba mpya, tatizo la Tanzania ni UTII wa Katiba iliyopo. Tumekosa watu wenye kuitii Katiba yetu ndio maana inaonekana mbovu. Katiba hata ikiwa mpya, bora kwa namna gani kama haikufuatwa na kuheshimiwa haina maana yoyote.

Hii ndio sababu wenye HOJA hii, tunashauri watu wafundishwe kutii Katiba kisha tunaweza kufikiria kuandika Katiba mpya. Kuandika Katiba mpya katika nchi ya watu wasio na desturi ya kutii Katiba ni kupoteza muda bure kwa kuwa hata hiyo mpya itavunjwa vilevile, itakosa maana.

Katika kusaidia jambo hili, tumewaeleza wenzetu kwamba jambo la Katiba ni la msingi sana lakini limefanywa kwa haraka mno bila maandalizi ya kutosha kwa hivyo litakwama. Tumewaeleza kuwa, mambo makubwa kama haya huhitaji maandalizi ya kutosha kabla ya kuanzishwa kwake. Tumewapa mfano wenzetu kwamba, hata katika uumbaji, Mungu alipokusudia kumuumba binadamu hakuanza na binadamu bali mazingira yake kwanza. Aliumba nuru na giza, anga na ardhi, maji na mimea kwa ajili ya chakula na maji ya kunywa. Halafu mwishoni akamuumba Mwanadamu, akamaliza kazi yake kwa ufanisi.

Kama Mungu angalianza kumuumba Mwanadamu kabla ya nchi, Mwandamu angalikosa mahala pa kuishi. Au kama Mungu angalitangulia kumuumba Mwanadamu kabla ya mimea na maji, bila shaka Mwanadamu angalikosa maji ya kunywa na chakula cha kula. Angalikufa na kazi ya Mungu ingalikosa maana

Huwezi kudai Katiba mpya bila kwanza kuwafundisha watu utii wa Katiba kwa sababu watavunja Katiba iliyopo ili kupata Katiba mpya. Ni kosa hilo!! Sio jambo la hekima kudai Katiba ya nchi nzima kwa kutegemea akaunt ya Kigogo Twitter au Maria Sarungi. Ni ukorofi kumtegemea Mdude Nyagali katika madai ya Katiba mpya kwa sababu Katiba ya nchi ni zaidi ya umbea na matusi. Katiba ya nchi ni jambo kubwa kabisa katika nchi lenye kuhitaji akili kubwa na utulivu wa hali ya juu. Wenye madai haya kwa sasa, wamekosa sifa hizi. Hawawezi kupata chochote!!

Pengine nioneshe udhaifu wa HOJA zinazotumiwa katika madai ya Katiba mpya ambazo zingaliweza kutatuliwa na UTII wa Katiba iliyopo;

1. Mamlaka ya Rais
Wanasema kuwa Rais amepewa mamlaka makubwa sana na Katiba hii. Nadhani, hawakufikiria sawasawa katika madai haya. Rais wa nchi ni kama Baba wa familia, mamlaka ya Rais katika nchi ni sawa na mamlaka ya Baba katika familia. Anawajibika na kila kitu kama msimamizi na mwamuzi mkuu wa familia. Ni kosa kusema Baba amepewa mamlaka makubwa katika kutimiza wajibu wake isipokuwa ikiwa atatumia mamlaka hayo vibaya. Hata ikiwa hivyo, kosa haliwezi kuwa na mwenye kutoa mamlaka isipokuwa mwenye kuyatumia vibaya. Tufundishe watu utii wa Katiba iliyopo.

Katika kuipa uzito hoja yao hii, wanatumia ibara ya 37(1) kuwa Rais atakua huru na hatalazimika kuchukua ushauri wa mtu yeyote isipokuwa kwa matakwa ya Katiba. Kwa sharti hili, Katiba haimlazimishi Rais kuchukua ushauri wa mtu lakini pia haimzuii Rais kushukua ushauri mzuri wa mtu yeyote. Kuna kosa gani katika Katiba yenye kumpa uhuru Rais katika kushauriwa na yeyote na isiyomzuia kukubali kushauriwa. Bila shaka tatizo haliwezi kuwa Katiba bali utii wa Katiba. Hatuwezi kuwa na Katiba inayomlazimisha Rais wa nchi kuchukua ushauri wa mtu kwa sababu tunaweza kuwa na Ma-Rais wengi kwa wakati mmoja. Rais mwenye kukataa ushauri mzuri ametumia vibaya uhuru wa Katiba sawa na Rais mwenye kuchukua ushauri mbaya. Katiba inayompa Rais uhuru wa kuchagua ushauri wa kuchukua kulingana na maslahi ya nchi haiwezi kuhesabika kuwa Katiba mbaya. Tuwafundishe watu UTII wa Katiba!

2. Tume huru ya Uchaguzi
Kuna kosa gani katika Katiba inayounda Tume ya Uchaguzi na kuweka sharti kwamba Tume haitalazimika kufuata amri au maagizo ya mtu yeyote au idara yoyote ya Serikali au Chama chochote cha Siasa” (Ibara ya 74(11)). Kuna kosa gani na Katiba ya namna hii??

Tumesema, tatizo la nchi yetu sio Katiba mpya bali UTII wa Katiba. Mwenyekiti wa Tume anayefuata maagizo ya Kiongozi wa Serikali amevunja Katiba kama Kiongozi wa Serikali au Chama cha Siasa anayemwagiza Mwenyekiti wa Tume kitu cha kufanya. Katiba imekataza tayari, imeweka katazo kwa vyovyote hili haliwezi kuwa kosa la Katiba isipokuwa watu wasiotii Katiba ya nchi na kuwa tayari kuisimamia. Katiba inayozuia Chama cha Siasa kuingilia shughuli za tume halafu Chama kikaingilia kwa maksudi, Katiba inayoizuia Serikali kuingilia shughuli za Tume ya Uchaguzi ina kosa gani? Tunataka Katoba mpya ifanyeje ifanyeje matika hili? Hapana. Narudia, tatizo letu sio Katiba mpya bali utii wa Katiba iliyopo. Kama watu wataamua kuitii, kuiheshimu na kuisimamia Katiba hii, tunaweza kuwa na Katiba bora kuliko inavyofikiriwa.

3. Ukuu wa Katiba
Wenye kudai Katiba mpya, wanasema Katiba iliyopo inavunjwa hovyo. Wanatolea mfano Wabunge 19 walioko Bungeni kinyume na utaratibu. Ndio maana nasema watu hawa hawajui hata wanachokidai. Sasa kama Katiba iliyopo inavunjwa hovyo suluhu ni kupata Katiba mpya au kuzuia watu wasivunje Katiba. Hivi, kuna kosa gani katika Katiba inayotaja sifa za Mbunge (Ibara ya 67 (1) (b) kuwa lazima awe na Chama cha Siasa halafu Spika wa Bunge kwa maksudi akaruhusu Wabunge wasio na sifa kushiriki Bunge.

Tunawezaje kuilaumu Katiba kwa kosa hili ambalo imeliwekea utaratibu na sheria. Kama Spika wa Bunge angalitii Katiba hilo lisingalikuwapo. Narudia tena, tatizo letu sio Katiba mpya bali utii wa Katiba iliyopo. Kama watu hawakufundishwa KUTII Katiba, hata ikipatikana Katiba mpya namna gani haiwezi kuwa namaana yoyote. Itavunjwa kama inavyovunjwa hii.

#TufundisheUtiiWaKatibaKwanza.
MenukaJr.
FikraHuru!

Chanzo: Jamii Forums