Categories
Maoni Siasa

Maoni Kuhusu “Mtu Asiyejulikana” Kuchukua Fomu ya Chadema ya Ubunge Kibamba: Hujuma au Maigizo?

Moja ya matukio ambayo yameendelea kutawala anga za habari za uchaguzi nchini Tanzania ni hilo la fomu za ubunge wa jimbo hilo kwa upande wa Chadema kuchukuliwa na “mtu asiyejulikana.” Gazeti hili lilisharipoti kuhusu tukio hilo japo jana sakata hilo lilichukua sura mpya baada ya kusambazwa video inayoonyesha suala zima.

Na ni video hiyo inayoweza kuashiria kuwa huenda suala zima ni “mchezo wa kuigiza.” Haihitaji “jicho la kijasusi” kuona tangu mwanzo wa video husika kwamba ni kama wahusika walijua kuna nini kitatokea. Lakini pia ikumbukwe kuwa taarifa hii ilisharipotiwa na aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungu, Boniface Jacob

Lakini hata kama si “mchezo wa kuigiza,” kwanini Chadema hawajajifunza walichofanyiwa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana ambapo kulikuwa na utitiri wa hujuma dhidi ya chama hicho katika zoezi la kuchukua na kurudisha fomu? Katika mazingira haya, Chadema walipaswa kuwa “watu wa kwanza” kuchukua fomu mara baada ya utaratibu huo kuanza. Ni kama ule utaratibu wa tahadhari ambapo mtu anayetaka kusafiri anaamua kulala stendi ili asichelewe basi.

La muhimu zaidi kwa chama hicho sio tu kuwatafuta “wachawi wao” bali pia kuhakikisha kuwa hakuna fursa yoyote ile inayoweza kutumiwa na CCM au mapandikizi wake kukihujumu chama hicho kikuu cha upinzani

ANGALIZO:

Maoni haya hayamaanishi ndio mtazamo wa gazeti hili.