Categories
Habari

@ZittoKabwe Amuomba Mama @SuluhuSamia Kusaidia Kuachiwa kwa Mbowe

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Zitto Kabwe amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kusaidia kuachiwa kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Zitto ambaye pia ni kiongozi wa Chama Cha ACT-Wazalendo ametoa ombi hilo leo wakati wa mkutano wa wadau wa kujadili hali ya demokrasia ya vyama vingi nchini.

Mbowe na wenzake watatu wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 16/2021 yenye mashtaka sita yakiwemo ya kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi, inayoendelea katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Akizungumza kwa sauti ya upole Zitto amesema, “Sisi viongozi wa vyama tupo hapa na wengine hawapo kwa sababu zao lakini kuna mwenzetu hayupo hapa kwa sababu ya changamoto za kisheria.

Tuna utamaduni wa kumaliza haya mambo na haitakuwa mara ya kwanza, tunakuomba sana kwa mujibu wa sheria na kufuata taratibu tusaidie mwenzetu tuwe naye ili tuweze kufanya kazi kwa pamoja na kuunganisha nchi yetu, tufanye siasa za tija na maslahi kwa nchi yetu,”. Amesema Zitto nakuongeza

“Ni dhahiri kuna changamoto za hapa na pale na wewe ndio Rais wetu, tunakuomba sana kama ambavyo uliahidi katika hotuba yako ya kwanza wakati unazindua Bunge.

“Utuunganishe, tumepalanganyika, uliweke taifa pamoja na nina amini una uwezo wa kuliweka taifa pamoja na utaliweka taifa pamoja tunakuomba sana mama,”

Kuhusu mkutano huo wa wadau kujadili hali ya demokrasia nchini, Zitto amesema ni hatua kubwa katika kuelekea kuwa na majadiliano ya kisiasa.

“Sisi tunachukulia kuwa hii ni hatua muhimu katika kuelekea kuwa na majadiliano ya kisiasa katika nchi yetu, huu ni mwanzo mwema.

“Kila jambo lina mwanzo na huu ni mwanzo mwema, ninaamini Mungu atatuongoza kuwa na utaratibu wa kujadiliana na kutatua changamoto zetu kwa majadiliano,” amesema Zitto.

CHANZO