Categories
Habari

Wanafunzi Vyuo Vikuu Walizwa Mamilioni ya Upatu, Wahusika Wa Kampuni Iliyofanya Utapeli Wadai Walikuwa na Baraka za Serikali

Mamia ya watu wanaoshiriki upatu unaoendeshwa na kampuni ya Alliance in Motion Global Tanzania (AIM-Global) wameingiwa wasiwasi wa kupoteza mamilioni ya fedha walizowekeza katika kampuni hiyo kwa matarajio ya kuvuna zaidi.

Kuendesha upatu ni kinyume cha kifungu cha 171A (1) na (3) cha Kanuni ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa mwaka 2006.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa wanafunzi wengi wa vyuo vya elimu ya juu wamewekeza fedha zao katika kampuni hiyo iliyosambaa katika mikoa kadhaa nchini.

Septemba 8, mwaka huu Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro lilitangaza kuwa liwashikilia wafanyakazi sita wa Kampuni ya Allince in Motion Global kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya utapeli.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Said Mtanda ndiye aliamuru wakamatwe baada ya kupokea taarifa kuwa zaidi ya watu 50 wameitwa na kampuni hiyo kupatiwa ajira wakati si kweli.

Mtanda alisema wanafunzi hao badala ya ajira huishia kupewa semina ambayo hulipia Sh220,000 kila mmoja, kiasi ambacho aliagiza kirejeshwe ili warudi makwao.ADVERTISEMENT

Kampuni hiyo yenye makao yake makuu Mikocheni, Dar es Salaam, kwa mujibu wa nyaraka za usajili inajishughulisha na kuuza kwa mtandao (network marketing) virutubisho vinavyotengenezwa Ufilipino na kuingizwa nchini.

AIM-Global ilisajiliwa na Wakala ya Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) mwaka 2016 ikiwa na mtaji wa Sh10 milioni na inamilikiwa kwa hisa na raia watatu wa Ufilipin – Raymond Asperin, Eduardo Cabantog na Francis Miguel.

Soma zaidi: Vijana 500 wafukuzwa Kilimanjaro baada ya kutapeliwa

Usajili huo, hata hivyo, haujabainisha shughuli kuu ya kampuni hiyo, bali imesajiliwa kufanya “shughuli nyingine binafsi za huduma.”

Wanafunzi walalamika

Ufuatiliaji wa Mwananchi umebaini kuwa wanafunzi kadhaa wameingiwa na hofu ya kupoteza fedha walizowekeza katika kampuni hiyo kwa matarajio ya kupata zaidi.

Baadhi ya washiriki ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Tumaini, Kampasi ya Dar es Salaam (Turdaco), ambao hutumia fedha zao, hasa za mkopo wa elimu, kuwekeza kwenye biashara hiyo. Wasiwasi wao ni uwezekano wa kupoteza fedha zao kufuatia taarifa kuwa kampuni hiyo inaendesha upatu kwa kivuli cha biashara kuu ya virutubisho.

Soma zaidi:Sita washikiliwa kwa kufanya utapeli wa ajira Moshi

“Wana mtindo wa kualika mwanachuo mmoja kutoka chuo chochote, ukifika wanakupa karatasi, wanakwambia andika majina ya wenzako ambao wanapokea mkopo, ukiwaandika wanakwambia utoe Sh580,000 na kupitia wao utakuwa unaingiza Sh50,000 kwa kila mtu atakayetoa fedha kama hizo (Sh580,000),” alieleza mwanafunzi mmoja kwa sharti la kutotajwa jina. Baadhi ya wanafunzi hao wanahoji bila majibu mfumo huo wa kuingiza fedha bila kufanya kazi au zinapotoka fedha za kuwalipa pale watakapoingiza watu wengi.

Wamesema wanapojaribu kuhoji, wahusika huwaambia ‘hayo msimweleze mtu yeyote zaidi ya kumleta hapa ofisini.’

“Mimi nilialikwa na mwenzangu, ukifika pale baada ya kuelezewa mfumo huo wa kupata fedha kwa njia ya kualika wenzako, unaambiwa usiwaambie chochote mpaka wafike ofisini ili wajionee wenyewe,” anasema mwanafunzi mwingine.

Mwananchi limebaini pia kampuni hiyo inaendesha shughuli hizo katika mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro na Arusha tangu mwaka 2019, ikiwalenga wanavyuo na wanafunzi waliomaliza kidato cha sita.

“Mwaka 2019 nikiwa Mwanza, wafanyakazi wa hiyo kampuni walinifuata ili nijiunge nao, kwa kuwa sikuwa na hela za kutoa ilinibidi nimuombe baba lakini alikataa. Kwa kuwa niliamini ni fursa, nilitoa hela ya fomu ya kujiunga (Sh30,000) na nikaanza kuhudhuria semina zao.

“Ukiangalia shuhuda za watu waliojiunga, hakuna hela yoyote wanayopata. Kwenye mfumo wao wanakuonyesha hela zipo zinasoma, lakini ukifuatilia kuzitoa kila siku utaambiwa mtandao unasumbua na huwezi kuzipata,” alidai mwanafunzi mwingine.

Shuhuda mwingine aliyeomba kutotajwa jina alisema aliweka fedha zote zinazohitajika katika kampuni hiyo na tangu mwaka 2019 mpaka sasa haoni faida yoyote aliyopata.

“Nilijiunga mwaka 2019 kwa kushawishiwa na rafiki yangu, lakini mpaka leo sijarudishiwa hela yangu na sijawa tajiri wala sijamiliki magari kama walivyonielezea. Na watu wengi wanajitoa kwa sababu hawaoni matokeo yoyote,” alisema.

Mwanafunzi mwingine aliyedai kuwekeza katika kampuni hiyo ameviomba vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kuhusu uwekezaji wa kampuni hiyo.

“Kwa kweli tuko gizani, hatujui hatima ya fedha zetu maana minong’ono imeanza kuwa hii nayo ni kama Deci (kampuni ya upatu iliyodhibitiwa na fedha zake kufilisiwa). Vyombo vya dola vitutoe wasiwasi,” alisema mwanafunzi huyo wa UDSM.

Baraka za Serikali

Mmoja wa viongozi wa kampuni hiyo, Alex Kisanga ameliambia Mwananchi kuwa kampuni hiyo imekuwepo nchini kwa zaidi ya miaka mitatu na inaendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Tumefuata taratibu zote za kufanya shughuli hii ya network marketing (uuzaji wa mtandaoni). Tuna kila kitu. Kampuni yetu si ya kijanjajanja.

Tunafanya network marketing katika nchi zaidi ya 56 duniani. Bidhaa zetu zimethibitishwa na tunalipa kodi TRA,” alisema Kisanga, ambaye hata hivyo alidai si msemaji wa kampuni hiyo.

AIM-Global inaendesha biashara katika sura mbili – kuuza virutubisho vinavyotajwa kusaidia wagonjwa mbalimbali na kuendesha biashara ya upatu (pyramid scheme).

Kila Jumamosi, AIM-Global hufanya kongamano linalowakutanisha watu wa aina mbalimbali, hasa wanafunzi wa elimu ya juu, kwa kile wanachoeleza kuwa ni kuwafungulia njia ya ajira baada ya kuhitimu masomo yao kwa kuzingatia ugumu wa kupata ajira.

Kisanga anasema asilimia 80 ya mafanikio ya biashara hiyo inatokana na mtandao wa biashara ya upatu wakati biashara ya virutubisho imechangia asilimia 20 tu ya mafanikio yao.

Mtu anapoingia anatakiwa kuwekeza Sh580,000 na baada ya hapo atatakiwa kuingiza watu wawili au zaidi kwenye mtandao huo ili afuzu kulipwa Sh50,000 na kadiri mnyororo unavyoongezeka, mtu wa kwanza kukaribisha wengine atakuwa akivuna Sh85,000 endapo wawili aliowaingiza nao wataingiza watu wengine.

CHANZO