Categories
Habari

Ubungo Wampima Ubavu Mama Samia: Baada Ya DC, Madiwani Kunusurika Kuzichapa, Meya Na DED Waparurana Hadharani

KIKAO cha Baraza la Madiwani la Manispaa ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, kilichofanyika jana Jumatano, tarehe 19 Mei 2021, kiliingia dosari, baada ya kuibuka mvutano kati ya Meya wake, Songoro Mnyonge na Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Sipora Liana. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es salaam…(endelea).

Mvutano huo uliibuka, baada ya Sipora kutuhumu katika manispaa hiyo, kuna genge la wezi, akidai kuna mtandao wa wizi wa fedha za ushuru wa takakata.

Kufuatia tuhuma hizo, Songoro alimtaka Sipora alifichue genge hilo la uhalifu, ili vyombo vya ulinzi na usalama, vichukue hatua.

“Kutumia kauli ya kusema kuna genge la wezi wa Manispaa Kinondoni, wewe ni mkurugenzi, inawezekana na wewe ni sehemu ya wezi. Mimi ni Meya inawezekana na mimi nikawa sehemu ya genge la wezi, ukisema hapa ni genge la wezi inawezekana na madiwani nao ni genge la wezi,” alisema Songoro.

Songoro alisema, kama Sipora angepeleka ushahidi juu ya tuhuma hizo katika vikao vya baraza hilo, zingefanyiwa kazi na Mkuu wa Polisi Wilaya Kinondoni (OCD), maafisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambao wanashiriki vikao hivyo.

Sipora Liana kuwa, mkurugenzi mpya wa Manispaa ya Kinondoni

“Kama kuna hilo genge la wezi naomba utuletee hilo genge ni la kina nani na katika vikao vyetu, tunavyofanya kama hivi vya baraza kuna watu wazito yupo OCD humu ndani , RPC, Afisa Usalama wa Taifa, Takukuru,” alisema Songoro na kuongeza:

“Suala sio kupeleka mtu polisi, suala kupeleka mtu polisi kwa ushahidi ili kama anatuhuma apelekwe mahakamani. Ndiyo tunachotaka sisi, lakini suala la kusema tuna genge, inawezekana tukakaa miaka mitano tunazungumza habari ya magenge.”

Baada ya kuzungumza hayo, Sipora aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam ambapo baada ya kuvunjwa, alihamishiwa Kinondoni, aliutaja mtandao huo akisema, kuna tabia ya baadhi ya watendaji wa manispaa hiyo, kufanya udanganyifu katika ukusanyanji fedha za takataka.

Sipora alidai, alifanya uchunguzi na kubaini, wananchi hupewa risiti zenye kiwango kidogo cha fedha tofauti na fedha halali wanazolipa.

“Wale watu walikuwa wamepewa kazi ya kukusanya mapato ya takataka, wakawa wanatoza wananchi Sh.2,000, Sh.1,000 na Sh.3,000 lakini risiti wanazotoa zimeandikwa Sh.100, Sh.200 na Sh.300. Wananchi wakaandamana kuja ofisini kwangu wakaleta risiti,” alisema Sipora

Alisema “nikatuma watu wangu kuchunguza wakabaini ni kweli wananachi wamelipa Sh.1,000, Sh.2,000 na Sh.3,000. Tukaja kwenye mfumo wa kaprinti kuanzia mwaka jana Julai, tukaona katika kila risiti wamechukua Sh.900, Sh.1,800 na Sh.2700.”

Chanzo cha habari: Mwanahalisi