Categories
Habari

Mdau Ashauri TONY BLAIR Aulizwe Kuhusu Ahadi Yake ya MWAKA 2013 Kusambaza ‘Sola’ Shule za Sekondar za Vijijini Tanzania

Mdau mmoja huko Jamii Forums amehoji kuhusu ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza mwaka 2013 ya kusambaza sola katika shule za sekondari za vijijini nchini Tanzania.

Ifiatayo ni habari husika ya mwaka 2013 kuhusu ahadi hiyo.

Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair ameahidi kuangalia uwezekano wa kuzisaidia shule za sekondari za vijijini katika Tanzania, kwa kuziwekea umeme wa nguvu za jua ili nazo zianze kunufaika na teknolojia ya kisasa katika masomo.

Aidha, Bw. Blair ameahidi kuwa atasaidia Tanzania katika mapambano yake ya kuongeza upatikanaji wa umeme nchini na pia kuwa atatoa mchango wa kuboresha Mpango wa Utekelezaji kwa Haraka (PDU), ambao umeanzishwa ili kuiwezesha Serikali kuongeza kasi na uwezo wake wa kutoa huduma na kutimiza ahadi zake kwa wananchi.

Waziri Mkuu huyo wa zamani amezitoa ahadi hizo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, mkutano uliofanyika Ikulu, Dar Es Salaam.

Bw. Blair ambaye yuko katika ziara ya baadhi ya nchi za Afrika amesema kuwa ahadi hizo kwa Tanzania zitatekelezwa kupitia taasisi yake mpya ya Tony Blair Africa Governance Initiative (agi).

Kabla ya kuja Tanzania, Blair ambaye anafuatana na mkewe Cherie Blair alitembelea nchi za Guinea, Sierra Leone, Liberia na baada ya kutoka Tanzania atakwenda Malawi.Katika mkutano huo uliochukua kiasi cha saa moja na robo, Rais Kikwete amemwelezea kwa undani kabisa jitihada zinazofanywa na Serikali yake katika maeneo ya uchumi kwa ujumla na katika sekta mahsusi kama vile miundombinu, mapambano dhidi ya mfumuko wa bei, Reli, Bandari za Dar Es Salaam, jitihada za kujitegemea kwa chakula na usalama wa chakula nchini, sekta ya maji, uzalishaji umeme na jitihada za kuongeza kasi katika eneo hilo, elimu, afya na PDU.

Uongozi wa Tony Blair ulikuwa moja ya Serikali za mwanzo duniani kuanzisha utaratibu wa Mpango wa Utekelezaji kwa Haraka na Waziri Mkuu huyo wa zamani ameipongeza Serikali ya Rais Kikwete kwa kuanzisha mpango huo.Amesema kuwa Mpango huo unaipa Serikali ya Tanzania nafasi ya kuelekeza nguvu zake ikiwamo bajeti na raslimali nyingine katika maeneo machache yenye uwezo wa kuleta mageuzi ya haraka katika maisha ya wananchi.

Blair amenukuliwa akimweleza rais Kikwete “Mh. Rais, napenda nikupongeze sana kwa uamuzi wako wa kuanzisha Mpango huu. Ni mpango ambao niliubuni katika Uingereza katika kipindi changu cha pili cha miaka mitano baada ya kufanya thathmini ya kipindi cha kwanza na utekelezaji wa Serikali yangu katika kipindi hicho”.”Mh. Rais, kila mtu anakubali kuwa ukiondoa Afrika Kusini na Nigeria ni Tanzania chini ya uongozi wake inayopewa nafasi kubwa zaidi ya kupiga hatua kubwa za mabadiliko na mageuzi katika Bara la Afrika.