Categories
Habari

Kuna Idadi Kubwa Ya Watoto Wenye Jinsia Mbili, Lakini Wanafichwa Na Wazazi, Hivyo Kushindwa Kupatiwa Matibabu.

MAMLAKA ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imesema kuna kundi kubwa la watoto wenye jinsia mbili, lakini wanafichwa na wazazi, hivyo kushindwa kupatiwa matibabu.

Kutokana na hatua hiyo,  jamii    imetakiwa  kuacha imani potofu na kutumia fursa zilizopo katika mamlaka hiyo, ili watoto hao wafanyiwe uchunguzi kubaini jinsia yenye nguvu na kujengewa uwezo.

Akizungumza katika Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimatafa (DITF),  yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Udhibiti anayesimamia uingizaji, usambazaji na matumizi ya kemikali nchini, Daniel Ndiyo, alisema kundi kubwa la watoto wenye jinsia linafichwa.

“Mamlaka kwa kushirikiana na madaktari mbalimbali nchini,  inafanya uchunguzi kwa watoto wanaozaliwa na jinsi mbili tofauti, lengo ni kuangalia  ipi ina nguvu na inaweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi,”alisema. Alisema wakati umefika jamii kuacha kuwaficha watoto hao na kuwapeleka katika mamlaka ya mkemia mkuu ili kufanyiwa uchunguzi.

Ndiyo alisema watoto wanaozaliwa na jinsi mbili tofauti wapo na wamebaini wanafichwa,  hivyo  ni vyema wananchi kujengewa uwezo wa elimu na kubaini kuwa hilo ni tatizo la kawaida hivyo waache imani potofu.

“Kwa sasa hakuna haja ya kuwaficha watoto hao, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali inatoa huduma za kiuchunguzi na  ile  inayothibitika  inatawala kati ya kiume na kike, inajengewa uwezo na kufanya kazi,”alisema

Alisema  uchunguzi wa kimaabara una uwezo wa kutambua kuwa mtoto huyo ni mwanamke au ni mwanaume na  jinsi ipi ambayo haitakiwi kuwepo na wataalamu wa mkemia mkuu wanawashauri madaktari kufanya upasuaji, ili kumwezesha mtoto huyo atambulike kama ni mwanaume au mwanamke.

Pia, aliongeza mamlaka hiyo inafanya uchunguzi wa vinasaba kwa wagonjwa wa figo na kutafuta ndugu ambaye vinasaba vinashabihiana ili kufanya matibabu.

“Tunafanya uchunguzi  kuthbitisha iwapo ndugu wanaotaka  kutoleana figo, kama zinawiana na kuwashauri madaktari kabla ya kufanya  upasuaji wa upandikizaji,” alisema.

Alisema katika masuala hayo ya uchunguzi wa figo wamekuwa wakishirikiana na hospitali mbalimbali nchini, ikiwemo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Aga Khan.

Ndiyo, alisisitiza kuwa  mamlaka hiyo inatekeleza sheria ya masuala ya usimamizi na udhibiti wa kemikali mbalimbali  zinazotengenezwa na kuingizwa nchini.

Alieleza lengo la kushiriki maonyesho ya mwaka huu ni kuikumbusha jamii majukumu ya  GCLA na ikiwemo uchunguzi wa kimaabara wa sampuli mbalimbali.

Alitaja baadhi ya sampuli za jinai ni pamoja na masuala yanayohusiana na ubakaji, wizi, dawa za kulevya, sumu na sampuli za kijamii na kuthibitisha ubora wa maji mara baada ya kuchimba kisima.

Chanzo: Uhuru