Categories
Habari

Kesi Ya Sabaya: Kama Ilivyotarajiwa, Ajitetea Kwamba Yote Aliyofanya Yalikuwa Maagizo Ya Rais Magufuli

Mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya unyang’anyi wa kitumia silaha na Kupora Mali na fedha ,Lengai ole Sabaya (34)ameiambia mahakama kuwa alitumwa na rais marehemu John Magufuli kuvamia duka la Shaahid Store ili kumkamata Mmiliki wa duka hilo, Mohamed Saad.

Akiongozwa na wakili Mosses Mahuna wakati akitoa utetezi wake mbele ya hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo wa mahakama ya hakimu Mkazi Arusha,Sabaya alidai yeye bado ni mtumishi wa Serikali ila alisikia tangazo la kusimamishwa kazi kutoka Kwa Rais Samia Suluhu.

Alidai kuwa siku ya tukio Februari 9 mwaka huu majira ya saa 9 kasoro alasiri alipigiwa simu na Mamlaka iliyomteua na kumpatia maelekezo ya kwenda kufanya kazi maalumu Arusha na kumtaka aongozane na watu wanne waliokuwa wakimsubiri uwanja wa ndege wa Kimataifa Kilimanjaro KIA.

Sabaya alidai kuwa walipofika Arusha wakiwa na wale watu wanne ambao ndio wenye taarifa zote walielekea eneo husika waliokuwa wameelekezwa na Mamlaka husika katika eneo la duka la Shaahid store lililopo mtaa wa Soko kuu jijini Arusha.

Akihojiwa na Wakili Mahuna kuhusu kazi aliyokuwa akiifanya kabla ya tarehe 9.2.2021 ,Sabaya alidai alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani kilimanjaro na aliteuliwa na Rais Hayati Dkt John Pombe Magufuli tarehe 29.7.2018.

Lengai Ole Sabaya anaeleza mahakama kuwa alitumikia wadhifa huo kwa kipindi cha miaka 2 na miezi 10 na alikoma kuhudumu wadhifa huo tarehe 13.5.2021 baada ya Rais Samia Suluhu kutengua nafasi yake kupisha uchuguzi .

Sabaya ameieleza Mahakama kwamba baada ya kufikia katika duka hilo walimkosa Mmiliki wa duka na ndipo alipowasiliana na mamlaka iliyomtuma kazi hiyo, ambayo ilimjibu kwamba imeshafanya mawasiliano na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Kenan Kihongozi na imeelekeza watu waliokutwa eneo la tukio wapelekwe kituo cha polisi kwa mahojiano zaidi ili kusaidia kupatikana Kwa mhusika wa duka aliyekuwa akitafutwa.

Anaeleza kuwa suala la yeye kupatiwa maelekezo na Mamlaka ya uteuzi ni Jambo la kawaida

kwani miezi mitatu kabla ya siku ya tukio 9.2.2021 alipewa maelekezo ya kufanyakazi maalum na kubaini mtambo wa kutengeneza fedha bandia na kukamata fedha bandia sh,milioni 800 jijini Dar es salaam.

Sabaya anaeleza kuwa katika zoezi hilo alikuwa msimamizi mkuu ambapo Hata Gavana wa Fedha Prof Florian Luoga pamoja na aliye kuwa waziri wa Fedha hapa Nchini Dkt Philp Mpango ambaye kwasasa ndiye Makamu wa Rais wanalijua.

Sabaya amedai kuwa hajawahi kufikia katika duka la Shaahid Store na kupora kiasi cha sh, milioni 2,769,000 na kisha kumpiga human Jasim , Bakari Msangi, Salim hasani na Ally shabani na kuwatisha Kwa silaha na kwamba hamfahamu mshtakiwa mwenzake anayetajwa Kwa jina la Daniel Mbura na pia Silvester Nyegu hakuwa naye siku ya tukio.