Categories
Habari

Hotuba ya Kamishna wa Fedha na Lojistiki wa Jeshi la Polisi, Kamishna Hamad Khamis Hamad katika uzinduzi wa jengo jipya la kituo cha polisi cha Mikokotoni, Kaskazini Unguja, Machi 25, 2022

Mh. Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja
Mh. Mbunge wa Jimbo
Mh. Mwakilishi wa Jimbo
Kamishna wa Polisi Zanzibar
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja
Wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na Usalama
Maafisa Waandamizi Makao Makuu ya Polisi Zanzibar
Maafisa, Wakaguzi na askari wa Mkoa wa Kaskazini Unguja
Mkandarasi Albatna Building Constructor L.TD
Mshauri Mwelekezi Samkay Consult CO L.T.D
Waandishi wa habari
Mabibi na Mabwana
Itifaki imezingatiwa
Assalam Alaykum,


Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia afya njema na kutuwezesha kukutana na mahali hapa leo, kwa ajili ya makabidhiano na uzinduzi wa jengo jipya la Kituo cha Polisi Mkokotoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja Kwa niaba na Mkuu wa Jeshi la Polisi naomba nitumie nafasi hii kwa heshima kubwa kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutimiza mwaka mmoja na kuendelea kuiongoza vyema nchi yetu katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita kwa mafanikio makubwa. Mh. Rais atabaki katika kumbukumbu za Jeshi la Polisi kwa mchango wake uliotukuka wa kulijengea uwezo Jeshi la Polisi katika maeneo yake yote; ajira, upandishwaji vyeo, mazingira bora ya kufanyia kazi, vitendea kazi na makazi kwa maafisa na askari.


Aidha, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa namna anavyoendelea kuiongoza nchi ya Zanzibar kwa mafanikio makubwa ambayo tunayaona. Tumuombe Mwenyezi Mungu awazidishie afya njema viongozi wetu ili waweze kutimiza azma ya kuwaletea wananchi maendeleo.


Nitowe shukurani za dhati kwa nyote mliohudhuria kwenye hafla hii. Shukrani za kipekee kwako Mh. Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ambae pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kaskazini Unguja. Natambua una majukumu mengi na muhimu ya kimkoa na kitaifa, lakini kwa kuthamini umuhimu wa kazi za Polisi na mchango wake katika shughuli za maendeleo umeamua kuungana nasi katika hafla hii, asante sana.


Jengo hili tunalokabidhiwa na kulizindua leo tarehe 25/03/2021, ni matokeo ya juhudi za Jeshi la Polisi zinazoendelea za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na makazi ya askari Polisi nchini. Jengo hili
imejengwa katika eneo ambalo hapo awali kulikuwa na Kituo cha Polisi kilichojengwa miaka ya 1950 kabla ya Mapinduzi matukufu mwaka 1964. Mwaka 2010 Kituo hicho kiliungua moto na kusababisha huduma za zilizokuwa zikitolewa Kituoni kuhamishiwa kwenye mabanda ambayo yalikuwa yakitumika kwa makazi ya askari. Hadi sasa hivi huduma hizo zinaendelea kutolewa kwenye mabanda hayo.

Mradi wa ujenzi wa Kituo kipya cha Polisi Mkokotoni ulianza rasmi tarehe 03/07/1912 takriban miaka 10 iliyopita. Mradi huu ulitarajiwa kukamilika ndani ya wiki 30 baada ya kusainiwa Mkataba baina ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kampuni ya ujenzi ya Albatna Building Constructor na Mshauri Mwelekezi wa mradi Samkay Consult Co. Ltd, zote za Zanzibar. Ujenzi wa jengo hili ulikwama mwishoni mwa mwaka 2012 kwa kukosa fedha. Hatua iliyokuwa imefikiwa ni kukamilika ujenzi wa boma lote na kupauliwa. Mradi huu hadi kukamilika kwake umegharimu kiasi cha shilingi 513,964,808.75.

Fedha zilizotumika kumalizia mradi huu ambazo ni shilingi 340,282,500.00, ni sehemu ya kiasi cha shilingi 4,190,666,010.00 zilizotolea na Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar peke yake katika kipindi cha kati ya mwezi wa Oktoba 2021 hadi mwezi Februari 2022. Kiasi hicho cha fedha kimetolewa kwa ajili ya kumalizia miradi ya ujenzi iliyokwama kwa sababu ya kukosa fedha na uanzishaji wa miradi mipya.

Miradi hiyo ni ujenzi wa Kituo cha Polisi Kizimkazi (198,934,710.00), ujenzi wa jengo la ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja (1,650,724,400.00), ujenzi wa jengo la ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Unguja (1,650,724,400.00), umaliziaji wa ujenzi wa nyumba za kuishi askari Mkoa wa Kusini Pemba (200,000,000.00) na umaliziaji wa ujenzi wa nyumba za kuishi askari Mkoa wa Kaskazini Pemba (150,000,000.00).

Shilingi 4,190,666.010.00 za miradi niliyoitaja, zinatoka kwenye mfuko wa Tuzo na Tozo wa Jeshi la Polisi ambao mapato yake hutokana na vyanzo vya ndani nje ya Jeshi la Polisi. Mapato yanayotokana na vyanzo vya nje, hukusanywa kutokana na huduma za ulinzi zitolewazo na Jeshi la Polisi kwa mabenki, taasisi, viwanda na migodi Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

Nitumie nafasi hii kwa niaba ya Jeshi la Polisi kuziomba taasisi zinazopata huduma zetu ziendeleekutuunga mkono na zile ambazo bado hazijaanza kutumia huduma hiyo zituunge mkono kwa sababu fedha tunazokusanya zinatumika kuboresha mazingira ya utendaji wa Jeshi la Polisi ambalo jukumu lake kubwa ni kulinda usalama wa raia na mali zao. Aidha, fedha hizo za miradi ambayo inatekelezwa kwenye maeneo mbalimbali hapa visiwani, hutoa ajira kwa ndugu zetu na kuchangia kuongezeka kwa mzunguko wa fedha kwa sababu vifaa vyote vya ujenzi na malighafi kwenye miradi hiyo hununuliwa hapa hapa Zanzibar.


Jitihada za kuboresha mazingira ya kazi na makazi kwa askari ndani ya Jeshi la Polisi ni endelevu. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 tunakusudia kuomba kiasi cha shilingi 1,368,720,550.00 kwa ajili ya miradi 15 ya ujenzi na ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi kwa ajili ya maafisa na askari Unguja na Pemba. Tunatarajia kiasi hicho kitaongezeka kutokana na miradi itakayotengewa fedha katika Mpango wa Matumizi wa mfuko wa Tuzo na Tozo kwa mwaka 2022/2023. Hapa nisisitize tena uungwaji mkono wa matumizi ya huduma za ulinzi zinazotolewa na Jeshi la Polisi ili kuongeza mapato ya mfuko kwa maendeleo ya Jeshi la Polisi na taifa kwa ujumla. Sotetunafahamu mazingira magumu ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.

Wakati tunafurahia makabidhiano na uzinduzi wa jengo jipya la Kituo cha Polisi Mkokotoni, nitumie nafasi hii kuwakumbusha askari wenzangu kwamba kituo hiki kitumike kama sehemu ya utatuzi wa shida za wananchi wa eneo hili na kwengineko zinazotokana na matendo ya kiuhalifu na matishio ya kihalifu yanayoleta kero kwa wananchi. Kituo hiki kisigeuzwe kuwa sehemu ya kubambika watu kesi (analetwa mtuhumiwa kwa kesi ya kuiba nazi, anapewa kesi mauaji), kusuluhisha kesi au kushughulikia kesi za madai. Aidha, kituo hiki kisitumike kama sehemu ya kugeuza haki kuwa batili na batili kuwa haki au wenye hatia kuachiwa huru na asiye na hatia kuadhibiwa. Badala yake kitumike kama kimbilio la wananchi wanaotafuta haki zao kisheria kwa mujibu wa sheria.

Aidha, niwakubumbushe askari wenzangu kwa ujumla kuonyesha uzalendo wa hali ya juu katika kutimiza majukumu yetu. Uzalendo wa askari Polisi kama mtumishi wa umma huonekana anapojitolea katika kutekeleza majukumu yake na kazi zake bila kujali shida zote. Tukiwa wasimamizi wa sheria, lazima tuheshimu utawala wa sheria na kuwa mfano wa kufuata sheria, kuheshimu haki za kikatiba, kutekeleza majukumu yetu bila woga wala upendeleo, kuhakikisha usawa mbele ya sheria, kuepuka chuki na ubaguzi wa aina zote, kuhakikisha uadilifu, kupinga rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na mamlaka tuliyopewa kisheria. Aidha, kuhakikisha
tunatekeleza majukumu yetu kwa namna na njia inayoamuru heshima inayostahili Jeshi la Polisi ndani na nje ya Jeshi lenyewe.

Kwa upande mwengine niwaombe wananchi wa Mkokotoni na visiwa vya Zanzibar kwa ujumla, kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwanza kwa sisi wenyewe kufuata sheria za nchi ili kuepuka kuingia mikononi mwa vyombo vya dola. Wahalifu tunaishi nao, hivyo tuwe tayari kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi tunapobaini viashiria vya uhalifu ili vidhibitiwe kwa mujibu wa sheria kabla havijaleta madhara kwa mtu mmoja mmoja au kwa watu wengi. Aidha, mtutambuwe askari Polisi kama sehemu muhimu ya jamii tunaofanya kazi muhimu ya kijamii, hivyo, tunahitaji ushirikiano wenu wa hali na mali katika kutanzua uhalifu na matishio ya uhalifu katika nchi yetu.

Kabla sijahitimisha hotuba hii, nichukue nafasi hii kuipongeza Kamisheni ya Polisi Zanzibar kwa usimamizi mzuri wa miradi inayoendelea visiwani Zanzibar. Niwapongeze Mkandarasi Albatna Building Constructor Ltd. na Mshauri elekezi Samkay Consult Co. Ltd kwa uzalendo mlioonyesha hadi kukamilika mradi huu pamoja changamoto nyingi zilizojitokeza.

Mwisho, kabla ya kutamka kulizindua rasmi jengo hili, napenda nikumbushe utunzaji wa rasilimali zetu zikiwemo majengo, samani, vyombo vya moto na kadhalika. Rasilimali hizi zinagharimu Serikali fedha nyingi ambazo zingetumika katika maeneo mengine yenye uhitaji mkubwa kwa ustawi wa nchi na raia wake. Nitowe rai kwa uongozi wa Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar na Makamanda wa Polisi Mikoa yote ya Tanzania Bara, kuhakikisha hatua za kisheria na kinidhamu zinachukuliwa ipasavyo bila hiyana kwa yeyote atakaethibitika kuharibu au kusababisha uharibifu wa rasilimali kwa makusudi au uzembe. Hatua hizo zitasaidia kuweka nidhamu katika matumizi ya rasilimali tunazokabidhiana kwa madhumuni ya kutekeleza majukumu yetu kisheria.

Baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, sasa natamka rasmi leo tarehe 25/03/2022 jengo jipya la Kituo cha Polisi Mkokotoni nimelifungua rasmi.

ASANTENI KWA KUNISIKILIZA