Categories
Habari

Dear Mama Samia, Unahujumiwa Huko TRA

Bandiko la mdau huko Jamii Forums

Rais wangu, ukipata nafasi mwite ofsini Kamishna wa TRA nchini, Bwana Alphayo Kidata. Muulize katika mwezi April/May ambao yeye amekua ofisini amekusanya mapato kiasi gani. Akikupa hesabu linganisha na mwezi wowote katika mwaka wowote unaoutaka wewe. Achana na miaka ya JPM ambayo inasemwa kodi zilikusanywa kwa nguvu. Tumia mwezi wowote katika kipindi cha awamu ya nne kwa makadilio. Ukipata majibu, mpe nafasi ya mwisho Alphayo Kidata, aache kukuchezea!!

Rais wangu, TRA ya Tanzania haikusanyi kodi tena. Wanafika ofsini kwa muda, wanakaa kidogo katika meza zao zilizopangwa shaghalabaghala, wengine wanawasha kompyuta wengine hawawashi. Baada ya muda mfupi, wanakusanyana nusu yao wanaondoka. Wao wanasema wanakwenda kufanya kazi za nje. Ndugu Rais, TRA ya Tanzania inafanya kazi za nje kwa ajili ya kazi za ndani zisizokuwepo.

Rais wangu, wakati wote huu wote waliobaki ofsini, hawana cha kufanya. Waranda-randa ofsini na kupiga miayo na soga. Wengine wanasimulia habari za msiba wa JPM. Hakuna lolote linalofanyika kwa sababu hakuna mtandao. TRA hawakusanyi pesa kwa sababu ya mtandao, nchi haikusanyi mapato kwa sababu ya mtandao. Tatizo la mtandao wa TRA limekua sugu katika nchi yetu, linajirudia leo, kesho na keshokutwa. No one cares!! Mtu mmoja ameniambia kuwa jana (May, 26) TRA nchi nzima haikufanya kazi. Yaani kwamba, kwa siku nzima nchi yote haikukusanya mapato kupitia chombo chake kikuu cha makusanyo. Kama taarifa hii ni ya kweli basi tatizo ni kubwa. Nchi hii siku hizi haikusanyi pesa, halafu inatumia pesa zilizokusanywa na wengine. Wenye hofu wanasema zikiisha zilizokusanywa nchi inaweza kuanguka.

Rais wangu, nenda leo TRA Mwenge, TRA Tegeta na TRA Kimara (zote za Da’slama), kwa kuzitaja chache. Ukikuta zote zinafanya kazi na inaonesha zimefanya kazi yake ipasavyo kwa siku tatu nyuma au na zaidi, niwajibishe mimi kwa namna utakayoona inafaa. Tuna tatizo kubwa, katika nchi kubwa namna hii kushindwa kukudanya mapato kwa sababu ya mtandao ni aibu. Huu utaratibu usipoangaliwa, nchi itatufia mikononi. Nchi isiyokuwa na mapato yake haiwezi kulipa mishahara kwa wakati, haiwezi kununua dawa za hospitali, hakwezi kugharamia elimu bila malipo na haitoweza kukamilisha miradi ya maendeleo ya gharama kubwa. Tukiruhusu nchi ifike hapo, ndio tumekwenda na maji tayari.

Rais wangu, juzi mtandao wa Tanesco ulisumbua kidogo katika kununua LUKU. Licha ya taarifa iliyotolewa mapema na Tanesco ya kuomba radhi lakini nchi nzima ilisimama. Waziri wa Nishati akahamaki, akafukuza watu hovyo, Waziri Mkuu akasimama kutoa maelekezo. Baada ya muda mfupi, umeme ukarudi. Tanesco haikusanyi mapato kama TRA lakini tuliwekeza nguvu kubwa usiku na mchana. Mtandao wa TRA hauna uhakika kwa zaidi ya mwezi, unasumbua kila siku lakini hakuna anayejali, Waziri wa fedha hajulikani alipo wala hajali.

Rais wangu, ni kama wote tumeridhika na hali hii. Pesa hazikusanywi kwa wakati kwa sababu ya mtandao, watu wanakwenda TRA na kurudi kila siku halafu muda wa kulipa ukipita mfanyabiashara anatozwa faini (penalty) kwa kuchelewa kulipa kodi. Hivi ndivyo tunavyohuisha bishara na kuvutia wawekezaji katika nchi yetu. Mtu kwenda TRA kulipa kodi moja kila siku ni kero, tunaharibu ratiba za watu bila sabbau. Wanaomkumbuka Magufuli wanamkumbuka kwa mengi, sisi tuendelee kufanya kazi za nje tukirudi ndani nchi itakua hoi bin taaban. Rais wangu, TRA watakukwamisha ukiweza chukua hatua sasa

MenukaJr,
Da’slama-Tanzania.

Chanzo: Jamii Forums