Categories
Habari

Baada Ya Kukumbana Na Misukosuko Ikiwa Ni Pamoja Na Kukamatwa na Kuhojiwa TAKUKURU Mara Baada Ya Kurejea Tanzania, Manji Aamua Kurudi Tena Ughaibuni

Mfanyabiashara Yusuf Manji amerejea ughaibuni baada ya kukaa nchini kwa takribani mwezi mmoja huku akikumbana na misukosuko baada ya kukamatwa na kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kisha kuachiwa kwa dhamana.

Taarifa zilizolifikia Mwananchi na kuthibitishwa na watu wa karibu wa Mwenyekiti na mfadhili huyo wa zamani wa klabu ya Yanga,  zinaeleza kuwa aliondoka nchini mwanzoni mwa mwezi uliopita Julai  akielekea Afrika Kusini aliko mpaka sasa na kwamba kuna uwezekano ikamchukua muda zaidi kurejea tena nchini.

Soma zaidi hapa: Yusuf Manji mikononi mwa Takukuru

Jumapili Agosti 1, 2021 Mkurugenzi  Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni aliiambia tovuti ya Mwananchi  kuwa uchunguzi dhidi ya Manji unaendelea na yupo nje kwa dhamana, lakini anaruhusiwa kusafiri.

“Unajua bado tunaendelea na uchunguzi wetu kuhusu Manji na kama unavyojua yupo nje kwa dhamana ambayo haimbani kusafiri, ” alisema Hamduni na alipoulizwa kama Manji yupo nchi ama la na kama alitoa taarifa za kusafiri alisema,  “Sina uhakika kama amesafiri ama la.”

Manji, aliyeondoka nchini mwaka 2018, alirejea nchini Juni Mosi na baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) alishikiliwa na maofisa wa Takukuru kwa mahojiano

Mfanyabiashara huyo aliyeshikiliwa kwa siku nne na Takukuru ikielezwa kuwa ana tuhuma tatu, ikiwemo ya kuisababishia Serikali hasara kwa kukwepa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika biashara yake na Shirika la Umeme nchini (Tanesco), baada ya kuachiwa kwa dhamana moja ya shughuli alizoshiriki ni mkutano mkuu wa klabu ya Yanga na ndio tukio pekee aliloonekana hadharani na kuzungumza.

Tuhuma nyingine zinazomkabili ni udanganyifu wakati wa ununuzi wa hisa za kampuni ya Tigo ambayo tayari imeuzwa kwa kampuni nyingine ya Madagascar na udanganyifu katika mapato ya klabu ya Yanga.

Licha ya tuhuma hizo, Manji aliamua kurejea nchini, jambo ambalo wachambuzi wa masuala ya siasa, biashara na utawala bora walisema halingewezekana bila mwelekeo wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi sambamba na kuishukia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) akiitaka kurekebisha mfumo wake wa ukusanyaji kodi ikiwa ni pamoja na kuzifungua akaunti za wafanyabiashara.

Watu wake wa karibu walilieleza gazeti hili kwamba alirejea nchini kutokana na kutokuwa na wasiwasi na mambo yanavyokwenda na jana wakalieleza Mwananchi kuwa ameondoka kwa sababu kuna vitu anaona havijakaa sawa.

Akizungumza na Mwananchi siku ya Jumapili kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wa watu wa karibu wa mfanyabiashara huyo alisema; “Aliondoka Julai mwanzoni yupo Afrika Kusini kwa sasa.”

“Mambo ya hapa (Tanzania) hayawezi kuna vitu vinaendelea ameona aondoke kidogo ila mwanawe bado tupo nchini.”

Alieleza kuwa akiwa Afrika Kusini, Manji anaendelea na biashara zake akisisitiza kuwa anaweza kurejea nchini ila si kwa sasa.

Chanzo: Mwananchi