Categories
Uncategorized

Tamko kamili la Baraza La Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) kuukataa mkataba wa bandari

“Ndugu zangu nawasihi mjihadhahari na wote wanaoleta mafarakano na vipingamizi kinyume cha mliyopokea (mapokeo). Waepukeni.Kwa maana watu kama hao wanatumikia tamaa zao kwa kutumia maneno matamu ya kudanganya kupotosha mioyo ya watu wanyofu” (Warumi 16:17-18). Sisi Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania,

 1. Tunatambua kuwakwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977), “Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo – (a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii; (b) lengo kuu la Serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi; (c) Serikali itawajibika kwa wananchi; (d) wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba” (Rejea Ibara 8, ibara ndogo 1); hivyo ni lazima Serikali iwasikilize wananchi.
 2. Kwa kutambua kwamba mamlaka ya Serikali yanatoka kwa wananchi, sisi Maaskofu wa Kanisa Katoliki la Tanzania, tumezisikiliza sauti zao, tumeisikiliza Serikali, na wadau wengine wa maendeleo,tukasali na kutafakari, na hivi tunatamka ifuatavyo:

2.1. Tukizingatia yaliyojiri na yanayoendelea katika jamii ya Tanzania tangu Mkataba huu uwekwe hadharani, taharuki kutokana na mijadala ya hadharani, mijadala ambayo imeligawa Taifa.

2.2. Na tukizingatia kuwa si mara yetu ya kwanza kutoa matamko kama hili kuhusu masuala yanayohusu jamii yetu;

2.3. Na kwa kurejea ibara za Mkataba tajwa hapo juu ambazo zina utata kwa uwekezaji wenye tija kwa Watanzania wa sasa na vizazi vijavyo;

2.4. Na tukiwa tunayashuhudia mashinikizo ya marekebisho ya sheria yanayokusudiwa kufanywa ili kuulinda Mkataba huu ambao Bunge la Tanzania limeuridhia hali tukiona ukiukwaji wa utawala wa sheria.

KWA HIYO:

 1. Tukisukumwa na dhamiri iliyo na lengo la kulinda rasilimali, mshikamano, amani, uhuru, na umoja wa kitaifa; tunathubutu kusema kuwa baada ya miaka 63 ya uhuru wa nchi hii, wananchi hawajapenda kuiachia bandari ya Dar es Salaam apewe mwekezaji mmoja aiendeshe,kwa vile Watanzania wenyewe wana uzoefu wa kuiendesha.
 2. Tunaona kuwa ni muhimu sasa kuendelea kujenga uwezo wa KITAIFA, kwa sekta zetu za umma na binafsi za Kitanzania tukiweka ubia na makampuni yenye ubobezi wa kiteknolojia kutoka sehemu mbalimbali duniani, na siyo ubia wa kutoka nchi moja, tukitumia mikataba yenye tija tuliyoandaa wenyewe juu ya mashirika yetu ya kibiashara.
 3. Tunakiri kuwa utaratibu wa Serikali kuweka wawekezaji kutoka nje tu katika njia kuu za uchumi umetukosesha uendelevu wa vitega uchumi vyetu hasa pale wawekezaji wanapoondoka. Hivyo, bandari ikiwa ni moja ya njia kuu na ya asili ya uchumi inayotuwezesha kufanya biashara kubwa na mataifa mbalimbali, ni lazima iendelee kuwa biashara ya Watanzania wenyewe na ibaki mikononi mwetu hata kama tunaingia ubia wenye tija.
 4. Kwa kurejea jitihada tulizofanya kuelewa Mkataba huu na kutoa ushauri wetu ambao haujazaa matunda mpaka sasa,na tukirejea mikutano yetu na Serikali katika ngazi za juu, ya tarehe 12 na 26 Juni mwaka huu 2023:

6.1. Tumefuatiliakwa umakini mijadala, maoni, mapendekezo na vilio vya wananchi walio wengi, ambao ni wamiliki wa bandari na rasilimali zote, na tumetambuakuwa wananchi walio wengi hawautaki Mkataba huu ambao unampa mwekezaji wa nje mamlaka na haki ya kumiliki njia kuu za uchumi kama zilivyobainishwa kwenye Mkataba huu.

6.2. Tumebaini kuwa kama nchi tumeshawekeza na kuendeleza bandari, reli, na bandari kavu huku tukiziendesha wenyewe.Hii ndiyo shauku ya wananchi, kusudi tuendelee kujenga uwezo wetu. Hali kadhalika, tumegundua mapungufuyetu ya uendeshaji wa bandari;vile vile tunao uwezo wa kuendelea kujizatiti kurekebisha mapungufu yanayojitokeza, wakati njia za kiuchumi zikibaki mikononi mwetu.

6.3. Kuna mifano tosha jinsi Watanzania tulivyoweza kujenga uwezo katika kuendesha mabenki kama vile NMB na CRDB, taasisi nyeti za umma na za binafsi na kadhalika.

 1. Sasa kwa vile wananchi walio wengi hawataki uwekezaji wenye masharti mabovu kama haya katika bandari zetu zote; na kwa kuwa Serikali inawajibika kwa wananchi, lazima viongozi wasikilize sauti ya watu, kwani sauti yao ni sauti ya Mungu.
 2. Historia imetufundisha kuwa kupuuza sauti ya wananchi kuhusu mikataba kwa siku za nyuma, kumeisababishia nchi hasara kubwa za kiuchumi, ukosefu wa ajira, na mapato ya kuendeshea huduma muhimu kama vile afya, maji na elimu. Tunashuhudia sasa Serikali kutokuwa na uwezo wa kuajiri na kulipa wafanyakazi wa kutosha katika sekta za elimu na afya ijapokuwa wahitimu wa fani hizo wako mitaani bila ajira. Hii ni kwa sababu vyanzo vikubwa vya mapato, mathalani migodi ya madini, vimemilikiwa na kuendeshwa na wawekezaji kutoka njekwa mikataba mibovu.
 3. Kupuuza sauti ya wananchi juu ya uwekezaji usiosikia sauti yao. kumewaletea pia wananchi wa maeneo wanayoishi mateso, kama inavyoonekana kwa jamii za Wamasai wa Loliondo, ambao haki zao za kiutamaduni na kijamii zimekiukwa. Uwekezaji umepewa kipaumbele kisicho na tija na raia wa Kimasai wameachwa wakiteseka.
 4. Tumeutafakari kwa makini Mkataba huu. Mkataba huu umechochea mgawanyiko wa wananchi katika kupambana na ukiukwaji mkubwa wa utawala wa sheria, kutozingatiwa uhuru wa taasisi za kidemokrasia na mwingiliano wa mihimili yadola hasa Serikali na Bunge na sasa Mahakama inanyemelewa. KamaWatanzania tunapenda kusema kwamba bila uhuru wa taasisi hizi na utawala wa sheria tutaliangamiza Taifa.
 5. Ikumbukwe kwamba, kutokana na mjadala mpana wa suala hili la mwekezaji mmoja kwenye bandari za Tanzania, wananchi wenye mawazo tofauti hawajui wamwendee nani ili misimamo yaoiweze kusikilizwa na kuzingatiwa; kwani Wabunge ambao ni wawakilishi wao wamewatelekeza kwa kufungamana na mwekezaji mmoja, kutokana na Bunge kuridhia Mkataba huu mnamo tarehe 10 mwezi Juni, 2023.
 6. Hivyo, sisi Maaskofu Katoliki Tanzania wenye jukumu la kusimamia ustawi wa kila mwanadamu tunamwomba Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mamlaka aliyo nayo asitishe wasilisho la ridhio hili kwa upande wa pili,na vile vile Bunge nalo lifute ridhio la Mkataba huu unaolalamikiwa.
 7. Makubaliano haya ya Kiserikali (Inter-Governmental Agreement IGA yana hatari zifuatazo kwa nchi yetu:

13.1. Kuharibu umoja na amani ya nchi yetu. Tukumbuke amani ikivunjika, yaweza kurudi tena baada ya jitihadi ya vizazi vingi. Nchi jirani kadhaa zimethibitisha hili.

13.2. Rasilimali za nchi zinazolindwa kwa pamoja kuwanufaisha baadhi ya raia na hivyo kuleta ubaguzi wa kiuchumi kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 27

Ibara ndogo ya 1, inayosema “Kila mtu ana wajibu wa kulinda maliasilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi…”

 1. Ibara zifuatazo za Mkataba huu zina matatizo yatakayosababisha nchi kutofikia uhuru wa kiuchumi (economic independence):

14.1. Ibara ya 2 (1): inayohusu lengo la Mkataba huu ambalo ni kuweka utaratibu unaoibana Tanzania kisheria katika kuendeleza, kuboresha na kuendesha bandari zote za bahari na maziwa, maeneo maalum ya uwekezaji, maeneo ya usafirishaji wa mizigo, na maeneo mengine ya kiuchumi.

14.2. Ibaraya 4: inayohusu wigo wa Mahusiano na Utekelezaji unaoitaka Serikali ya Tanzania kuwajibika kuijulisha Dubai kila fursa ya uwekezaji inapojitokeza.Hiiinakinzana na baadhi ya sheria za nchi yetu, kwa mfanosheria ya ushindani na ile ya manunuzi.

14.3. Ibaraya 5: ambapo DPWorldimepewa haki ya kuendeleza, kusimamia na kuendesha miradi pekee yake, wakati Tanzania inabaki na wajibu wa kumwezesha kufurahia haki hiyo.

14.4. Ibaraya 6:inayoitaka Tanzania kuwajibika kuipatia DP World vibali na vivutio vya kutekeleza miradi yake kama Serikali. Hii inapingana na baadhi ya sheria za kiutaratibu.

14.5. Ibaraya 7: inayoitaka Serikali kuwajibika kutoa mamlaka yanayotakiwa na mwekezaji bila ucheleweshaji.

14.6. Ibaraya 8: Haki ya kutumia ardhi ambapo Mkataba unasababisha uvunjifu wa sheria za ardhi na sheria zinazohusu masuala ya ardhi.

14.7. Ibaraya 10: Usiri wa Mkataba ambapo Mkataba unazuia mamlaka nyingine kama TAKUKURU /BUNGE kufuatilia mikataba.

14.8. Ibara za 23 na 24: zenye ugumu wa kujitoa kwenye Mkataba.

HITIMISHO:

 1. Ni vyema, ni busara na ni hekima Serikali kuwasikiliza wananchi, maana kutowasikiliza ni kujiletea matatizo makubwa zaidi siku za usoni kwani wananchi hawahawa watavitaka vizazi vijavyo kuondokana na unyonywaji huu, kama tunavyoona kwenye kesi nyingi zinazoendelea sasa hivi katika mahakama za kibiashara za kimataifa dhidi ya mikataba iliyovunjwa na Serikali ya Tanzania. Tukumbuke mikatabaya madini miaka ya ’90 viongozi wa dini na asasi za kiraia walipinga uwekezaji wa namna hii, na Serikali ikatumia mamlaka zake kuridhia mikataba hii na tunashuhudia ikivunjwa na nchi kulipa fidia kubwa. sasa hivi
 2. Tunasisitiza kwamba SAUTI YA WATU NI SAUTI YA MUNGU, hivyo basi kuwasikiliza wananchi na kufanya maamuzi kadiri wanavyotaka kutailetea serikali heshima kubwa ya kuwa sikivu kwa watu. Kinyume cha haya, Mwenyezi Mungu anatuonya kupitia Nabii Yeremia anaposema: “Kama kapu lililojaa ndege walionaswa, ndivyo nyumba zao zilivyojaa mali za udanganyifu. Ndiyo maana wamekuwa watu wakubwa na matajiri, wamenenepa na kunawiri. Katika kutenda maovu hawana kikomo hawahukumu yatima kwa haki, wapate kufanikiwa, wala hawatetei haki za maskini” (Yeremia 5:27-28).
 3. Hivyo tukiwajibika kimaadili, tunaona ni jukumu la serikali kusikiliza wananchi wanaotaka mkataba huu ufutwe. Kwa kuwa tumeonesha kuwa Tanzania tumeshawekeza na kuendeleza bandari, reli na bandari za nchi kavu; niwajibu miradi hii tuiendeshe Watanzania wenyewe huku tukikaribisha ubia tunaoudhibiti wenyewe. Hiki ndicho wananchi wanachokililia kusudi tujenge uwezo wetu wenyewe. Kwa vile tumegundua mapungufu yetu ya uendeshaji wa bandari, tunaweza kujizatiti kurekebisha mapungufu hayo wakati njia za kiuchumi zikibaki mikononi mwetu. Kwa sababu hizo na maelezo yote ya hapo juu, sisi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania hatuungi mkono Mkataba huu.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.

Ni sisi Maaskofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania:

 1. Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga – Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
  Tanzania, na Askofu Mkuu wa Mbeya
 2. Askofu Flavian Kassala – Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
  Tanzania, na Askofu wa Geita
 3. Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya OFMCap – Askofu Mkuu wa Dodoma
 4. Askofu Mkuu Paul Ruzoka – Askofu Mkuu wa Tabora
 5. Askofu Mkuu Yuda Thadei Ruwa’ichi OFMCap – Askofu Mkuu wa Dar es
  Salaam
 6. Askofu Mkuu Damian Dallu – Askofu Mkuu wa Songea
 7. Askofu Mkuu Isaac Amani – Askofu Mkuu wa Arusha
 8. Askofu Mkuu Renatus Nkwande – Askofu Mkuu wa Mwanza
 9. Mwadhama Protase Kadinali Rugambwa – Askofu Mkuu Mwandamizi wa
  Tabora
 10. Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa – Askofu wa Iringa
 11. Askofu Severine NiweMugizi – Askofu wa Rulenge-Ngara
 12. Askofu Augustine Shao CSSp – Askofu wa Zanzibar
 13. Askofu Michael Msonganzila – Askofu wa Musoma
 14. Askofu Ludovick Minde ALCP/OSS – Askofu wa Moshi
 15. Askofu Method Kilaini – Msimamizi wa Kitume wa Bukoba
 16. Askofu Joseph Mlola ALCP/OSS – Askofu wa Kigoma
 17. Askofu Agapitus Ndorobo – Askofu wa Mahenge
 18. Askofu Rogath Kimaryo CSSp – Askofu wa Same
 19. Askofu John Ndimbo – Askofu wa Mbinga na Msimamizi wa Kitume wa Njombe
 20. Askofu Salutaris Libena – Askofu wa Ifakara
 21. Askofu Almachius Rweyongeza – Askofu wa Kayanga
 22. Askofu Liberatus Sangu – Askofu wa Shinyanga
 23. Askofu Titus Mdoe – Askofu wa Mtwara
 24. Askofu Eusebius Nzigilwa – Askofu wa Mpanda
 25. Askofu Bernadin Mfumbusa – Askofu wa Kondoa
 26. Askofu Prosper Lyimo – Askofu msaidizi wa Arusha
 27. Askofu Edward Mapunda – Askofu wa Singida
 28. Askofu Beatus Urassa ALCP/OSS – Askofu wa Sumbawanga
 29. Askofu Anthony Lagwen – Askofu wa Mbulu
 30. Askofu Filbert Mhasi – Askofu wa Tunduru Masasi
 31. Askofu Lazarus Msimbe SDS – Askofu wa Morogoro
 32. Askofu Simon Masondole – Askofu wa Bunda
 33. Askofu Henry Mchamungu – Askofu msaidizi wa Dar es Salaam
 34. Askofu Stefano Musomba OSA – Askofu msaidizi wa Dar es Salaam
 35. Askofu Wolfgang Pisa OFMCap – Askofu wa Lindi
 36. Askofu Christopher Ndizeye – Askofu wa Kahama
 37. Askofu Mteule Thomas Kiangio – Askofu mteule wa Tanga

Imetolewa Dar es Salaam,
Tarehe 18 ya Mwezi Agosti Mwaka wa Bwana 2023.

Mhashamu Askofu Mkuu Gervas Pd. Charles Kitima
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Katibu Mkuu wa Baraza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *