- Rais, mawaziri wakuu,viongozi wa mihimili yote ya serikali na gavana wa BoT
UNAPOUTAJA mwaka 1922, kipindi alichozaliwa Baba wa Taifa hayati Julius Nyerere, ni dhana inayoenda sambamba na kuanzishwa kwa shule ya sekondari Tabora Kwa lugha rahisi ‘wote ni wazaliwa wa mwaka mmoja’
TABORA HIGH-SCHOOL
Mbali na kugongana kwa mwaka huo wa kuzaliwa, ndiko Mwalimu Nyerere alikopata elimu yake ya sekondari, ambayo ina mchango mkubwa wa kumfikisha kwenye Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki wakati huo-Makerere kilichopo Kampala,Uganda.
Ikiwa ni shule maalum kwa ajili ya familia za machifu wakati huo wa ukoloni, mbali na Mwalimu Nyerere ,orodha ni ndefu iliyotoa majina makubwa yaliyotumikia taifa la Tanganyika na baadaye Tanzania.
Mkuu wa Shule hiyo, Robert Marwa alitaja katika orodha ya matunda hayo ya Tabora kuwa ni Waziri Mkuu wa Pili wa Tanganyika, Rashid Kawawa ambaye ana historia ndefu katika siasa ya nchi hii.
Pia yumo Cleopa Msuya ambaye katika vipindi viwili tofauti, alikuwa Waziri Mkuu na kutumikia nafasi nyinginezo nyingi za uwaziri kwa muda mrefu, sambamba na ubunge wa Mwanga kwa kipindi kirefu akiwa na mafanikio lukuki.
Naye, aliyekuwa mbunge wa Bunda na Jaji wa Mahakama ya Bahari kwa kipindi fulani, Joseph Warioba aliwahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais. Kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Sheria na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Marehemu Brigedia Jenerali Hashim Mbita, aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi wa Afrika (OAU) ambaye ana wasifu wa pekee hasa katika ukombozi wa Msumbiji, anaingia katika orodha ya wasomi hao.
Philemon Mgaya , aliyewahi kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi nchini katika miaka ya 1970 na kujijengea umaarufu mkubwa, mzizi wa maarifa na utendaji wake una chimbuko toka Sekondari ya Tabora.
Katika Bunge ambalo ni mhimili mwingine wa serikali, Spika wa Bunge marehemu Adam Sapi Mkwawa na Samwel Sitta, nao ni zao la Shule ya Sekondari Tabora.
Nao mhimili wa mahakama,ambao una jukumu la kutafsiri na kutoa maamuzi ya kisheria,wakuu wake ambao wana wadhifa wa Jaji Mkuu; Barnabas Samatta na mrithi wake Augustino Ramadhan (wote sasa wastaafu) ni wahitimu wa shule hiyo.
Chombo muhimu katika utendaji wa uchumi wa serikali, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambayo wiki iliyopita ilitimiza miaka 50 ya kuasisiwa kwake, mmoja wa gavana aliyewahi kuiongoza- Edwin Mtei, ni mhitimu wa Tabora.
Mbali na wasifu huo, Mtei anajulikana kwa umahiri wake wa uchumi wa kimataifa, pia ni muasisi wa chama maarufu wa upinzani nchini Chadema.
Katika ulingo huohuo wa kisiasa, msomi mahiri wa uchumi nchini na kimataifa , Prof. Ibrahim Lipumba ambaye aliwahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mara kadhaa kuwania urais katika uchaguzi mkuu nchini , naye ni mwana-Tabora School
Msomi mwingine na mwanasiasa kutoka shule hiyo ni Prof.Juma Kapuya, mwanazuoni wa elimu mimea wa UDSM na baadaye mbunge wa Urambo Magharibi aliyetumikia baraza la mawaziri kwa kipindi kirefu.
Wanasiasa wengine waliopitia shule hiyo ni,Oscar Kambona, Daudi Mwakawago, Job Lusinde, Basil Mramba, Joseph Butiku, Bakari Mwapachu, Joseph Mungai, Tuntemeke Sanga, Wilbert Chagula, Abubakari Mgumia, Nimrod Lugoe na Israel Elinawinga.
Mbali ya majina hayo makubwa ya kiserikali, shule hiyo ina umaarufu wake wa kipekee kwa kuzalisha wanasheria wengi mahiri nchini
Wasomi wa sheria nchini kama vile Prof.Issa Shivji na Mark Bomani ni matunda ya shule hiyo.
Historia ya Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora (Tabora Boys)
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, Robert Marwa, akizungumzia historia ya shule hiyo alisema kuwa, ilianzishwa mwaka 1922 wakati huo ikijulikana Tabora Central School.
Lengo la kuanzishwa shule hiyo ni kuwatayarisha watoto wa machifu na watu mashuhuri kuwa viongozi kwa kuwapatia stadi za kusoma, kuhesabu na kuandika ili kuwafanya wawe wasaidizi wa watawala wa kikoloni na katika uzalishaji.
Mwalimu Julius Nyerere akiwa mtoto wa Chifu wa Wazanaki, Nyerere Burito (1860–1942), alijiunga na shule ya sekondari Tabora mwaka 1937 na kuhitimu mwaka 1942
Marwa anasema aliyekuwa Kaimu Gavana na Mkuu wa Majeshi wa Tanganyika wakati huo, John Acott ndiye aliyeifungua shule hiyo mwaka 1925.
Baadaye shule hiyo ikaanza kuchukua watoto wa wananchi wa kawaida, hasa wale waliochaguliwa kwa kuonekana kuwa wana vipaji katika masomo hasa ya Hisabati na Kiingereza kutoka shule za kati zilizokuwa na madarasa ya tano hadi la nane.
Marwa anasema “mchakato uliofanywa kuwapata wanafunzi wa kuingia Tabora School ni kutoka katika mikoa na kufanya mahojiano na wanafunzi waliopendekezwa na shule kujiunga na Tabora School.Uteuzi wa viongozi wa wanafunzi ulifanywa kwa makini kubaini vijana wenye uwezo wa kuongoza wa kimasomo,”.
Sababu ya shule kung’ara ndani na nje ya nchi.
Pia Marwa alibainisha kuwa walimu waliwafuatilia wanafunzi kwa karibu tabia zao na kuwafungulia ukurasa wa pekee wa kila mwanafunzi ulioandikwa makosa yake, na kuwaadhibu au kuwapongeza mahali walipojipambanua kwa kufanya jambo zuri.
Kimsingi nidhamu ilisisitizwa kwa kuangalia jinsi mwanafunzi anavyotii taratibu ya shule na kutunukiwa nembo ya shule na beji ilipostahili.
Maendeleo ya shule ya wakati huo ni kwamba, wanafunzi waliokuwa wakifanya mitihani ya Cambridge matokeo yao yalikuwa ni ya daraja la kwanza na la pili.Waliopata daraja la tatu hawakufika hata robo ya darasa wakati huo.
Mwenendo huo wa shule wa kujivunia kwa mujibu wa Marwa uliifanya kujipambanua kuwa miongoni mwa shule za jumuia ya madola duniani, zilizokuwa zinafanya mtihani mmoja ili kupima uwezo wa wahitimu hao.
“Maandalizi ya wanafunzi hao ndio siri kubwa iliyowezesha wanafunzi kufanya vizuri katika mitihani yao pamoja na kule walikokwenda baada ya hapo kwa sababu walikuwa wamejengewa msingi mzuri wa kielimu,” alisema.
Shule ilikuwa imesheheni vifaa vya kufundishia na kujifunza kama vile vitabu vya kutosha kwa kila mwanafunzi na somo husika.
Pia maktaba ya shule ilikuwa na vitabu vya ziada na kiada, vilivyotosheleza mahitaji ya wanafunzi, ikiwamo aina ya encyclopedia, ambavyo ni vitabu vya kumbukumbu, maarifa na ujuzi.
Kama hiyo haitoshi , kulikuwa na maabara za kutosha zenye vifaa vya kumuwezesha kila mwanafunzi kufanya jaribio peke yake na kusaidiwa kuongozwa inapohitajika kufanya hivyo. Hiyo ilisaidia ubunifu na kuchochea ari ya kujifunza.
Kwa upande wa walimu kwa mujibu wa Marwa, walikuwepo wa kutosha kwa kila somo huku uwajibikaji wao wa ufundishaji masomo husika ulikuwa wa hali ya juu.
Ilikuwa vigumu sana kumkuta mwalimu anakosa kipindi au kuingia darasani baada ya dakika tano kupita. Nidhamu ilikuwa ya hali ya juu sana zama hizo.
Pia kwa upande wa wanafunzi, kila mmoja aliwajibika katika masomo kwa kuhakikisha kuwa, wanahudhuria vipindi vyote kwa wakati na wote walitakiwa kuwa wameketi kwenye viti vyao darasani kabla ya dakika tano kipindi kianze
Pamoja na malengo mengineyo,Tabora School ililengwa kuwaandaa watu watakaofanikisha utekelezaji wa ukuaji wa uchumi wa kikoloni hasa kupata mali ghafi kama vile pamba, tumbaku na katani
Shule ya kijeshi
Kwa miaka mingi shule hiyo hata baada ya uhuru iliendelea kufanya vizuri hata kuwa miongoni mwa shule zenye majina makubwa nchini kwa kuwapika wanafunzi kikamilifu.
Kutokana na hali halisi ya kisiasa nchini wakati huo, ilifanywa kuwa shule yenye mchepuo wa kijeshi uliwajengea wanafunzi ukakamavu na nidhamu ya hali ya juu pia kuwajaza uzalendo kwa nchi yao.
Wanafunzi walikuwa wanavaa sare za ‘kijeshi’ ( kombati za khaki kama za jeshi la mgambo), maafande wa Jeshi la Wananchi (JWTZ ) ndio waliokuwa wanaendesha mafunzo shuleni hapo kwa kuwapatia mwamko wa hali ya juu wa kuitumikia na kuilinda nchi yao.
Kabla ya kuanza masomo wanafunzi walipewa utambulisho wa kambi iliyojumuisha kwata za kijeshi na hatua nyingine wanazopitia ‘makuruta’ wanapoingia kambini kwa mara ya kwanza.
Na mwisho wa mwaka, wanafunzi wa kidato cha tatu na cha tano walipelekwa msituni kwa ajili ya mafunzo ya vita kwa vitendo, ikiwamo kufunzwa ujanja wa porini na zoezi la kulenga shabaha
Changamoto za shule sasa.
Robert Marwa alisema shule hiyo yenye madarasa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita ina wanafunzi 754.
Licha ya umaarufu mkubwa iliyonayo shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ambazo kwa namna moja au nyingine zinarudisha nyuma ufanisi wa malengo yake.
Mkuu huyo wa shule Marwa alisema, kwa upande wa mabweni kuna upungufu wa umeme, maji, uzio wa shule, vitanda, magodoro , zahanati hivyo kinachotakiwa ni kufanya ukarabati mkubwa ili kuirudisha shule katika hadhi yake ya kuwaandaa wanafunzi bora katika mazingira ya kuvutia na sio bora wanafunzi
CHANZO: Makala hii ilichapishwa Juni 28, 2016 katika gazeti la Nipashe