
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA na mkosoaji mkali wa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Dk Willbrod Slaa ametiwa mbaroni kwa tuhuma za uhaini.
Slaa alikamatwa siku ya Jumapili katika msako mkali wa serikali ya wakosoaji wa mkataba maarufu wa Tanzania na Dubai.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, kampuni ya kimataifa ya usafirishaji ya DP World yenye makao yake makuu Dubai, itachukua baadhi ya majukumu katika bandari ya Dar es Salaam, hatua ambayo imetajwa kuwa na manufaa kwa kampuni hiyo na si kwa nchi.
Aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Sweden alikamatwa nyumbani kwake Mbweni kabla ya kufikishwa katika kituo cha polisi cha Kawe kwa mahojiano.
Habari ambazo hazijathibitishwa zilisema kuwa Dk Willbrod Slaa alichukuliwa na polisi hadi nyumbani kwake baada ya kuhojiwa ili kufanya upekuzi kabla ya yeye mwenyewe kutangaza habari hizo kwenye programu ya kijamii ya Clubhouse.
“Nimepokea wageni hapa, baadhi ya maafisa wa polisi wameingia nyumbani kwangu, lakini sijazungumza nao,” alisema.
Wengine waliokamatwa kwa kukosoa mpango huo ni pamoja na Boniface Mwabukusi na Mdude Nyagali, madai ambayo polisi waliyakanusha kwanza kabla ya kufichua kuwa wako chini ya ulinzi na kwamba watafunguliwa mashtaka ya uchochezi.
Inspekta Jenerali wa Polisi Camilius Wambura alikuwa tayari ametishia kukamatwa kwa mtu yeyote atakayejaribu kuleta machafuko nchini.