Categories
Habari za Michezo

Mo atendewe haki, akiondoka Simba itayumba

Kwa mara nyingine Simba imemaliza ligi ya soka Bara bila ubingwa. Huu ni mwaka wa tatu mfululizo kwa timu hiyo kongwe kuambulia patupu. Mara ya mwisho Simba kuwa bingwa ilikuwa mwaka 2021.

Na katika miaka yote mitatu ambayo Simba imekosa ubingwa, watani zake wa jadi, Yanga, ndio wameibuka kidedea.

Kadhalika, katika misimu yote mitatu ambayo Simba imeshindwa kuchukua ubingwa, baadhi ya mashabiki wamekuwa wakimtupia lawama mfadhili mkuu wa klabu hiyo Mohammed “Mo” Dewji.

Hata hivyo, kuna namna mbili za kuangalia mchango na umuhimu wa Mo huko Simba.

Ya kwanza ni kwa kuangalia mafanikio mfululizo yaliyopatikana chini yake ambapo Simba ilichukua ubingwa wa Bara kwa miaka minne mfululizo, yaani mwaka 2018, 2019, 2020 na 2021.

Kila anayefuatilia soka la Tanzania, au kuielewa vema Simba atakwambia mafanikio hayo yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na ufadhili wa Mo.

Njia ya pili ya kutambua umuhimu wa Mo ni kuangalia mafanikio ya Yanga. Kwa kiasi kikubwa, mafanikio hayo yamechangiwa na ufadhili wa Gharib na GMS yake.

Swali linakuja, kama Mo aliweza kuleta mafanikio kwa ufadhili wake, na sasa Gharib analeta mafanikio Yanga kwa ufadhili wake, tatizo lipo wapi kwa Simba miaka mitatu hii?

Kinachoiangusha Simba sio Mo bali uongozi mbovu. Na licha ya ufadhili wa Gharib, jambo jingine linaloiletea mafanikio Yanga ni uongozi imara chini ya Injinia Hersi.

Na yayumkinika kuamini kuwa pindi Mo akichoshwa na lawama za wana-Simba, na kuamua kuondoka, basi uwezekano wa Simba kushika hata hiyo nafasi ya tatu waliyoambulia msimu huu utakuwa hafifu.

Wana-Simba wanapaswa kumwenzi Mo. Sambamba na hilo, kuna haja kwa klabu hiyo kuimarisha safu ya uongozi wake, iendane na spidi ya akina Injinia Hersi. Na katika hili, Mo ana nafasi ya kulifanyia kazi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *