Categories
Kimataifa Michezo/Burudani Siasa

Wasanii Tz Wana La Kujifunza Katika Mahojiano Haya Kati Ya Rapa Cardi B na Mgombea Urais USA Joe Biden

Moja ya habari zilizovuma kwenye vyombo vya habari vya Marekani ni mahojiano kati ya rapa maarufu wa kike wa Marekani, Cardi B na mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democrats, Joe Biden.

Kwa vile Tanzania nayo inajiandaa na kinyang’anyiro cha uchaguzi kama ilivyo Marekani, mahojiano hayo yanaweza kuwa funzo nzuri kwa wasanii mbalimbali nchini Tanzania, ambao wamekuwa mtaji muhimu kwa chama tawala CCM.

Machoni mwa wengi, wasanii hao wamekuwa wakionekana kama wanaojali maslahi yao binafsi na hata kushutumiwa kuwa “wanaendekeza njaa.” Lakini licha ya ushiriki wao wa mara kwa mara kwenye kampeni, wasanii hao huishia kusahaulika pindi uchaguzi ukipita.

Na japo takriban chaguzi zote zimeshuhudia wasanii wakijiweka karibu na CCM, uchaguzi wa mwaka huu unaweka rekodi ya kipekee ambapo licha ya kukikampenia chama hicho tawala, lundo la wasanii lilijitokeza kugombea uongozi japo asilimia kubwa walibwagwa kwenye kura za maoni.

Ni muhimu kutambua kama Watanzania wengine, wasanii hao wana uhuru wa kushabikia chama chochote kile. Hata hivyo, ajira za wasanii hao zinawategemea zaidi wananchi wa kawaida kuliko CCM au viongozi wake. Na kwa vile wasanii hao wapo karibu zaidi na wananchi kuliko viongozi wa CCM na/au serikali, ukaribu wao na viongozi hao wakati huu wa kampeni unaweza kuwa fursa muhimu kwao kufikisha ajenda za wanancho kwa viongozi hao.

Kwa bahati mbaya, kwa takriban wasanii wote, nafasi hiyo imekuwa fursa muhimu kwao kupiga mapicha na kusambaza mitandaoni wakiwa kwenye magwanda ya CCM. Japo ni haki yao kikatiba, yayumkinika kuwaona kama wasaliti kwa jamii ambayo sio tu ina matarajio kwao bali pia ndio inayowawezesha kuwa muhimu hadi CCM iwahitaji wakati wa kampeni.