Categories
Siasa

Wafuasi Wa “Shujaa Wa Afrika” Wamtishia Maisha CAG Kichere Kutokana Na Ripoti Yake Iliyoonyesha Ufisadi Mkubwa 2015 – 2020

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, ametishiwa maisha, baada ya ripoti yake aliyoitoa hivi karibuni kuibua madudu mengi yaliyogusa baadhi ya watumishi wa umma, Raia Mwema imefahamishwa.

Taarifa za ndani kutoka familia yake, zimethibitisha kuwapo vitisho dhidi ya CAG Kichere, ambaye kwa sasa ameimarishiwa ulinzi wa kawaida na wa kiintelijensia.

CAG Kichere ambaye alipata kuhudumu nafasi ya Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kabla ya kubadilishwa na kuwa Katibu Tawala wa Mkoa (RAS) wa Njombe, amekuwa na ulinzi wa kawaida, lakini siku za hivi karibuni baada ya kutishwa, aliongezwa ulinzi nyumbani kwake na ofisini.

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alikataa kuzungumzia suala hilo, kwa maelezo kwamba huyo ni kiongozi wa kitaifa, ambaye suala lake halipo eneo lake la kazi, na kutaka atafutwe Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime.

Hata hivyo, Misime alipopigiwa simu aliuliza: “nyie mmepata wapi hizo taarifa?” Na kukata simu bila kusema lolote.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Kichere hakupokea simu, na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi, hakujibu pamoja na kuulizwa kuhusu taarifa za kuwapo vitisho dhidi yake.

Raia Mwema haijathibitisha ni watu gani hasa waliotoa vitisho hivyo, pamoja na kuhusishwa kwa taarifa na kazi zingine za ukaguzi alizofanya Kichere kwa uadilifu mkubwa.

Hata hivyo, taarifa zinamnukuu Kichere akisema vitisho hivyo vinatokana na taarifa yake, iliyoibua madudu mengi.

“Hawa watu wanafanya madudu wenyewe, halafu wanamtishia CAG. Warekebishe au wajibu hoja zilizotolewa na kama kuna tatizo, wakubali kukabiliana na mkono wa sharia, si kumtisha mtu anayetimiza wajibu wake,” alisema mtu wa karibu na Kichere, kwa masharti ya kutotajwa jina gazetini.

Tangu ateuliwe kuchukua nafasi hiyo, CAG amekuwa akiibua madudu mengi ambayo yameibua mjadala mkubwa katika jamii, huku baadhi wakichukuliwa hatua.

Pamoja na ukaguzi mkuu wa kawaida, CAG amekuwa akifanya ukaguzi maalumu katika taasisi mbalimbali, kwa maelekezo ya Serikali, ikiwa ni pamoja na ukaguzi maalumu alioufanya mwaka jana kwenye Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), taarifa ambayo ilisababisha kusimamishwa kazi kwa watumishi kadhaa wa Mamlaka hiyo, na wengine kufikishwa mahakamani.

Katika taarifa yake kuu ya mwaka jana aliyoikabidhi kwa Rais Dk. John Magufuli, CAG aliibua madudu kadhaa ya TPA kabla ya kufanya ukaguzi maalumu.

Katika taarifa yake hiyo aliyoikabidhi Machi 30, mwaka jana, CAG alimshukuru Dk. Magufuli, kwa kuisaidia na kuipa nguvu ofisi ya CAG, iweze kutimiza majukumu yake ya kikatiba, kauli ambayo aliitoa tena alipokabidhi taarifa yake ya mwaka huu.

Aliyoibua 2021/22
Ripoti ya CAG, kwa mwaka wa fedha wa 2019/20, ilimweka matatani aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla.

Akitoa muhtasari wa ripoti hiyo Dodoma, Aprili 8 mwaka huu, CAG Kichere alisema, katika tamasha la Urithi Festival lililofanyika mwaka 2019, kulikuwa na viashiria vya ubadhirifu wa fedha kutokana na kanuni kadhaa kukiukwa.

Tamasha hilo lilifanyika chini ya uongozi wa Dk Kigwangalla akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Kichere alisema fedha zilizotumika kufanikisha tamasha hilo, hazikuwa kwenye bajeti ya Wizara hiyo, wala hakukuwa na mpango ulioidhinishwa wa utekelezaji wake.

Alisema kutokana na fedha hizo kuwa nje ya bajeti, Wizara hiyo ilichangisha Sh bilioni moja, kutoka kwenye wakala zake nne ambazo ni Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA).

“Hakukuwa na mpango wa utekelezaji wa tamasha la utalii, kutokana na kukosekana mpango wa utekelezaji uliodhinishwa, nilibaini kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii, iliomba wakala zake nne kuchangia,” alisema CAG.

“Kila moja ilitakiwa kuchangia Sh milioni 250 ambazo hazikuwa kwenye bajeti zao, ili kuwezesha kufanyika tamasha hilo,” alisema Kichere.

Kichere alisema ili kuongeza bajeti hiyo, Wizara ilichangia Sh. milioni 299 na Mfuko wa Fedha za Maendeleo ya Utalii Sh.
milioni 270.

Jumla ya Sh. bilioni 1.57 zilipatikana ili kufanikisha utekelezaji wa tamasha hilo, ambao fedha hizo hazikuwa kwenye bajeti za wizara wala taasisi husika.

Licha ya hayo, CAG alibaini kukosekana stakabadhi zinazothibitisha malipo ya Sh milioni 831.1 kutoka Wizara hiyo kwenda Kituo cha Televisheni cha Clouds na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

“Wakati wa utekezaji, nilibaini kuwa kituo cha Clouds na TBC walichukua Sh milioni 629.7 na Sh milioni 201 mtawalia, kwa ajili ya matangazo ya tamasha,” alisema CAG.

“Hata hivyo, hakukuwa na stakabadhi za kielekroniki kuthibitisha kupokewa kwa malipo hayo na waliolipwa,” alisema Kichere.

Pia alisema katika sakata hilo, kodi ya zuio kiasi cha Sh milioni 41 hazikukatwa katika malipo yaliyofanyika.

“Aidha, kodi ya zuio ya Sh milioni 31 na Sh milioni 10 kutoka Clouds TV na TBC mtawalia, haikukatwa kwenye malipo yaliyofanywa,” aliongeza CAG.

“Wizara haikupata hizo kodi ya zuio. Ushahidi unaonesha, kuwa ununuzi wa huduma za matangazo kwa TBC na Clouds, zilipatikana kwa njia ya ushindani usiosawa,” alisema Kichere.

Pia, CAG alisema katika ukaguzi wake alibaini, kwamba matumizi ya Sh milioni 478.26 katika taasisi saba, hayakuwa na nyaraka.

“Nilibaini jumla Sh milioni 487.26 zilipelekwa taasisi saba kwa ajili ya utekelezaji wa tamasha hilo. Hata hivyo, hakukuwa na nyaraka kwa ajili ya ukaguzi, kuthibitisha matumizi hayo,” alisema Kichere.

Mkaguzi huyo alisema, “hali kadhalika nilibaini matumizi ya Sh milioni 585.52 yaliyolipwa na Mhasibu wa Mfuko wa Tozo ya Maendeleo ya Utalii, bila kuwa na nyaraka toshelezi, hivyo nilishindwa kuthibitisha uhalali wa matumizi hayo.”

Katika hatua nyingine, CAG alisema katika ukaguzi wake, alibaini kiasi cha Sh milioni 140 kilitolewa na Wizara hiyo kwa maelekezo ya Dk Kigwangalla kwenda kampuni ya Wasafi, kinyume na Sheria ya Matumizi ya Umma.

Alisema, fedha hizo zililipwa kwa ajili ya wasanii wa kampuni hiyo kutangaza utalii wa ndani katika mikoa sita ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Dodoma, Kilimanjaro na Iringa.

“Nilibaini wizara ililipa Sh milioni 140 kwa kampuni ya Wasafi kwa ajili ya wasanii ambao wangetangaza utalii wa ndani, hakukuwa na mkataba wowote uliosainiwa kati ya kampuni hiyo na Wizara.

Hivyo, sikuhakiki wigo wa kazi pamoja na huduma zilizotolewa na kampuni ya Wasafi.

“Kulikuwa na maagizo ya Waziri yakielekeza malipo kwa Wasafi, katika mahojiano, Waziri alikiri kuwa kampuni hiyo iliomba zabuni ya kutangaza tamasha hilo katika mikoa iliyotajwa, na kutoa maagizo ya kutoelewa malipo hayo,” alieleza.

Alisema, kwa maoni yake kiasi cha Sh milioni 140 walicholipwa Wasafi kutokana na maelekezo hayo, hakiendani na sheria ya matumizi ya umma.

Bilioni 3/- zatengeneza ndege
CAG alibaini kuwa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA), ililipa Sh bilioni 3.92 kugharimia matengenezo ya ndege ambayo ilikuwa haifanyi kazi tangu mwaka 2015.

“Nilibaini, kuwa TGFA ililipa Sh. bilioni 3.92 Februari 14 na Aprili 26, 2018 ikiwa ni gharama za huduma ya matengenezo makubwa ya ndege aina ya Fokker 28-5H-CCM ya mwaka 1978,” alisema.

“Hata hivyo, wakati wa ziara yangu kwenye hifadhi ya ndege za Serikali Dar es Salaam Agosti 19, 2020, nilibaini kuwa ndege hiyo ilikuwa haifanyi kazi na ilikuwa imetelekezwa tangu mwaka 2015,” alisema Kichere.

Nyufa kwa DPP
Katika ripoti hiyo, CAG alibaini kasoro za kisheria na kikanuni za matumizi ya fedha, zilizotokana na mali zilizotaifishwa na kurejeshwa serikalini.

Alisema, alipitia uendeshwaji wa akaunti ya fedha zinazotokana na mali zilizotaifishwa na kurejeshwa serikalini, zilizo chini ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) hadi Juni 30, 2020.

Chanzo: Raia Mwema