Categories
Habari Siasa

Urais 2020: Hatimaye Lissu Apitishwa na Tume ya Uchaguzi kukabiliana na Magufuli

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania, Jaji Somistocles Kaijage ametangaza kuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu ametimiza vigezo vyote na masharti ya kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho kikuu cha upinzani .

Kulikuwa na hofu kubwa miongoni mwa wafuasi wa chama hicho kuanzia asubuhi baada ya Lissu kuwasili katika ofisi za Tume tangu saa 5 asubuhi kama ratiba ilivyoelekeza lakini mchakato ulichukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa huku Tume ikidai ilikuwa ikihaki wadhamini wa mwanasiasa huyo anayetarajiwa kutoa upinzani mkali kwa mgombea wa chama tawala CCM, Rais John Magufuli.

Kadri muda ulivyosonga mbele ndivyo hofu ilivyozidi kusambaa kuwa huenda Lissu amefanyiwa hujuma. Gazeti hili limebaini kuwepo kwa ahueni kubwa miongoni mwa wafuasi wa Lissu na Chadema kwa ujumla baada ya kufahamika kuwa mwanasiasa huyo amepitishwa rasmi kuwa mgombea urais.