Categories
Siasa

#Uchaguzi2020: Vyombo Vya Habari Vimekatazwa Kuripoti Habari za Chadema, ACT au Uoga Tu?

Kwa mujibu wa taarifa, kituo cha runinga cha Azam kiliweka bandiko kwenye ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Instagram, kisha ikafuta bandiko hilo. Hata hivyo baadhi ya wananchi walibahatika kuona bandiko hilo kabla halijafutwa.

Maelekezo Kutoka Juu au Uoga Tu?

Swali miongoni mwa wananchi wengi ni endapo kitendo hicho cha chombo hicho cha habari kilitokana na uoga tu au ni utekelezaji wa “maagizo kutoka juu.”

Hata hivyo, utafiti uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba sio Azam pekee ambao hawakuripoti tukio la mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu, kuchukua fomu za kugombea urais bali vyombo vyote vya habari vikuu (mainstream media) havikutangaza habari hiyo.

Kwa upande mwingine, vyama vya upinzani vimekuwa vikikabiliwa na ukiritimba katika usambazaji habari kwa vyombo vya habari visivyo rasmi, huku vikitegemea zaidi jitihada binafsi za vyombo hivyo ambavyo baadhi hutilia mkazo zaidi idadi ya wasomaji wa habari husika kuliko umakini wa habari husika.

Kwa muda mrefu vyama vya upinzani vimekuwa vikupuuza uwekezaji katika vyombo vya habari vyao binafsi, na tumeshu8hudia wakilitegemea gazeti la “Tanzania Daima,” ambalo sasa limefungiwa. Na hata gazeti hilo nalo halikuwepo mtandaoni kwa miaka mingi. Kati ya sasa na uchaguzi mkuu, ni lazima vyama hivyo vijenge mazingira yatakayowezesha habari zao kuwafikia Watanzania wengi Mwanahabari mstaafu aliyeomba jina lake lihifadhiwa

Kipaumbele Kwa Habari za Magufuli na CCM

Wakati habari za vyama vya upinzani zikikosa kuonekana kwenye vyombo vya habari vikuu, habari za mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli, zimetapakaa kila kona.

Japo Magufuli ananufaika kutokana na nafasi yake kama Rais, lakini pia yawezekana kuwa msisitizo wa vyombo vya habari kwenye habari zinazomhusu yeye, na viongozi wengine wa serikali ambao pia ni wana-CCM, ni maelekezo maalum kama yale ya kuzuwia urushwaji habari za vyama vya upinzani.

Na japo vyama vya upinzani vinaweza kupuuzia hali hii, baadhi ya wadau wameonyesha shaka kama kampeni za vyama hivyo zitakuwa na ufanisi wa kutosha hasa kwa vile sio rahisi wa wagombea wa chama hicho kufika kila sehemu.

Jitihada za gazeti hili kupata msimamo wa viongozi wa Chadema na ACT-Wazalendo zinaendelea.