Categories
Habari Siasa

Uchaguzi Mkuu Uganda: Tume ya Uchaguzi yawaonya Polisi

Tume ya Uchaguzi nchini Uganda imewatahadharisha polisi nchini humo dhidi ya kuwazuia wagombea wa urais kuendesha kampeni zao.

Tume hiyo imesema kuwa imepokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wagombea wa urais na pia kuona taarifa za vyombo vya habari kwamba polisi inazuia na kuvuruga kampeni zao.

Wakati huo huo, katika taarifa ya pamoja mabalozi wa nchi za Muungano wa Ulaya nchini humo, wameeleza kutofurahishwa kwao na ghasia zilizotawala kampeni ya uchaguzi tarehe 18 na 19, Novemba.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Uganda ilishuhudia ghasia na maandamano pamoja na matumizi yasiyofaa ya vikosi vya usalama dhidi ya raia, na kuvitaka vyama vyote vya kisiasa na wagombea wake kuwataka wafuasi wao kuacha ghasia na matumizi ya lugha mbaya.

Mabalozi hao wametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua kali za kisheria kumaliza uchokozi unaolenga kuleta ghasia au kusababisha ukiukaji wa sharia huku kiongozi wa upinzani k Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine akilalamikia kuzuiliwa kuendesha kampeni zake katika mji wa Hoima, Magharibi mwa nchi hiyo.

Katika ujumbe wake wa twitter, Bobi Wine amesema kuwa polisi walifunga barabara za kuelekea katika mji huo, ili kumzuia kufika katika hoteli aliyotarajia kupata malazi na kuziamuru hoteli zaote katika mji huo zisimpokee na timu yake, na hivyo kuwalazimisha kulala ndani ya magari.