Categories
Siasa

Rushwa Yachelewesha Vikao vya CCM Kupitisha Wagombea Ubunge

Ratiba za chama tawala CCM zinaonesha kuwa vikao vya Kamati Kuu wa CCM vilipaswa kufanyika Agosti 7 na 8 lakini hadi leo, takriban wiki sasa, hakuna kikao kilichoketi. Ajenda kuu ya kikao hicho ni kupitisha majina ya Wagombea wa Ubunge wa Majimbo wa CCM Tanzania Bara na Visiwani.

Kwa mujibu wa taarifa, sababu kuu iliyopelekea kuchelewa kwa vikao hivyo ni tuhuma lukuki za rushwa kwenye kura za maoni majimboni. Inaelezwa kuwa taarifa nyingi zimewasilishwa CCM kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Kamati ya Maadili ya CCM imeelemewa na wingi wa tuhuma hizo.

Katika suala hilo la rushwa, inaelezwa kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Rais John Magufuli, ni miongoni mwa wanaotaka “busara badala ya sheria” itumike katika kupata suluhu la jambo hilo. Kwamba, rushwa isiwe kigezo pekee cha kutopitisha wagombea bali waangaliwe kwa vigezo vinginevyo kama kukubalika. Inaelezwa kuwa japo kuna mvutano mkubwa katika suala hilo, hatimaye matakwa ya Magufuli yatatimizwa kwani uzoefu unaonyesha kuwa “busara zake zinapokwama, hutumia njia za kibabe kama vile kutishia wajumbe au kuihusisha Idara ya Usalama wa Taifa.”

Sababu nyingine inayotajwa kwa mujibu wa taarifa ni kilio cha wanachama kuhusu wanaostahili kupitishwa kwenye nafasi husika. Kuna waliokataliwa majimboni kwa sababu hawakutoa rushwa lakini wanatakiwa uongozini na wanachama. Kadhalika, kuna walioshinda kura za maoni majimboni lakini hawatakiwi na wanachama. Hata hivyo, japo wanachama hawa ndio wapigakura kwenye uchaguzi mkuu, sauti zao hazitarajiwi kuathiri maamuzi ya Magufuli ambaye ndiye mwenye maamuzi ya mwisho zaidi ya maamuzi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.