Categories
Habari Siasa

Nyalandu Azuiwa Kwenda Kenya Kwa Madai Ya Kutokuwa Na Nyaraka Muhimu

Aliyekuwa mgombea ubunge jimbo la Singida Kaskazini, (Chadema)Lazaro Nyalandu amezuiwa kutoka nchini kupitia mpaka wa Tanzania na Kenya wa Namanga baada ya kukosa nyaraka muhimu.

Akizungumza na Mwananchi leo, November 9, Mkuu wa wilaya Longido, Frank Mwaisumbe amesema mwanasiasa huyo alikuwa akitaka kuondoka nchini lakini hakukuwa na nyaraka zinazohitajika.

“Ni kweli maofisa wa uhamiaji mpakani wamemzuia kutoka nchini, kwani alikuwa hana nyaraka kadhaa ikiwamo za gari na vitu vingine ambavyo alikuwa anaondoka navyo,”amesema.

Amesema kwa sasa vitu alivyotaka kuvuka navyo bado vinashikiliwa mpaka wa Namanga na ametakiwa kuwasilisha nyaraka zake .

“Tumemtaka alete nyaraka muhimu zinazohitajika na tumemuachia akalete, lakini akishindwa atafikishwa mahakamani,”amesema.

Tukio hili limekuja wakati pia kukiwa na taarifa za aliyekuwa Mbunge wa Arusha mjini Godbless Lema kukamatwa nchini Kenya baada ya kuingia nchini humo bila kufuata taratibu huku ikidaiwa kuwa alikwenda kutafuta hifadhi kwa madai ya usalama wake.