Categories
Habari Kimataifa Siasa

Mama @SuluhuSamia asema katika baadhi ya maeneo, amefanya vema zaidi kuliko marais wanaume, aeleza changamoto alizokumbana nazo kama Mtanzania wa kwanza mwanamke kuwa Rais Tanzania.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kwamba katika baadhi ya maeneo, amefanya kazi vizuri zaidi kuliko marais wanaume waliomtangulia.

Ameeleza kuwa katika siku za awali za urais wake alikumbana na changamoto kutokana na kuwa mwanamke, lakini alimudu kuzishinda changamoto hizo.

Rais Samia aliongea hayo nchini Ghana, ambako anahudhuria mkutano wa kila mwaka unaoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ikiwa ni ziara yake ya kwanza kabisa ukanda wa Afrika Magharibi tangu aapishwe kuwa Rais, Machi 19 mwaka jana kufuatia kifo cha mtangulizi wake, John Magufuli.

Haikuwa rahisi kwa Watanzania kuniamini kwamba ningeweza kuongoza nchi kama wanaume wanavyoongoza – hiyo ilikuwa ni changamoto kubwa.

Katika mwaka (wa uongozi wangu) nimeonyesha nguvu za wanawake. Nimeongoza nchi katika namna ileile wanaume wanaongoza, na katika baadhi ya maeneo, nimefanya vema zaidi yao.

Rais Samia ndiye mwanamke pekee anayeshikilia nafasi hiyo barani Afrika. Urais nchini Ethiopia ambao unashikiliwa na mwanamke ni wa jina zaidi kuliko majukumu (ceremonial).

Alieleza kwamba uchumi wa Tanzania ulishuka kutoka asilimia 6.4 hadi asilimia 4 kutokana na janga la UVIKO-19, lakini chini ya uongozi wake, uchumi umekua hadi asilimia 5.2 huku ukitarajiwa kufikia asilimia 6.7 mwaka 2025

Mkutano huo unahudhuriwa pia na Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo, Filipe Nyusi wa Msumbiji na Azali Asoumani wa Komoro.

Leo, Rais Samia anatarajia kupokea tuzo ya “African Road Builders – Babacar Ndiaye Trophy” ambayo alitangazwa mwezi uliopita kuwa ndiye mshindi kwa mwaka huu

CHANZO