Categories
Siasa

Licha Ya Ahadi Kuwa Wangeshirikiana, Lissu Na Membe Kila Mmoja Kugombea “Kivyake.”

Vyama vikuu vya upinzani nchini Tanzania vimeshindwa kuunda ushirikiano uliotarajiwa kuvisaidia vyama hivyo kumng’oa madarakani Rais John Magufuli katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Jana ilikuwa siku ya mwisho kwa wagombea wa nafasi ya urais kutoka vyama mbalimbali kurejesha fomu zao Tume ya Taifa ya Uchaguzi huko Dodoma, na baadaye Tume kutangaza wagombea wa nafasi hiyo. Na katika taarifa rasni ya Tume hiyo, mgombea urais kwa tiketi ya Chadema Tundu Lissu atachuana sio tu dhidi ya mgombea wa CCM, Magufuli, bali pia wa chama cha ACT-Wazalendo, Bernard Membe.

Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi za nchi hiyo, mgombea urais atakayepata kura nyingi ndiye atakayetangazwa mshindi. Ni kwa sababu hiyo ilidhaniwa kuwa ushirikiano kati ya Lissu na Membe, kwa upande mmoja, na Chadema na ACT-Wazalendo, kwa upande mwingine, ungeweza kutenegenza mazingira mazuri ya ushindi kwa kambi ya upinzani.

Kutokana kila mmoja wao kusimamisha mgombea wao, kuna hatari vyama hivyo vikagawa kura dhidi ya Magufuli, ambaye pia anatarajiwa kunufaika kwa kura za vyama vingine “vinavyomuunga mkono,” kama vile NCCR-Mageuzi, CUF, TLP, nk.

Awali, kiongozi mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alinukuliwa mara kadhaa akidai chama chake na Chadema wangesimamisha mgombea mmoja. Hata hivyo, ilionekana bayana kuwa Chadema walikuwa hawana nia ya ushirikiano cha ACT-Wazalendo, pengine kutokana na ukweli kuwa Zitto alikataa kuungana na umoja wa vyama vinne vya upinzani, UKAWA, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.