Categories
Habari Siasa

Deodatus Balile: Magufuli Katutenda, Deni La Taifa Lafikia Sh TRILIONI 78, Mama Samia Msalabani.

Jamhuri October 26, 2021

Na Deodatus Balile

Kazi hii ya uandishi wa habari moja ya majukumu yake ni kuanika ukweli minong’ono inapotawala katika jamii.

Kwa sasa kuna minong’ono mingi. Minong’ono imeanza baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza hadharani mkopo wa Sh trilioni 1.3, alioukopa kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na akatangaza miradi lukuki itakayotekelezwa kwa kutumia mkopo huo.

Miongoni mwa miradi ya kihistoria ni ujenzi wa madarasa ya sekondari 15,000 nchi nzima na madarasa ya shule za msingi 3,000.

Kwa sasa inakadiriwa kuwa nchi ina upungufu wa madarasa 11,000, lakini Rais Samia ameamua kuona mbali.

Ameamua kufuta mfumo wa zima moto, ambapo kila mwaka wazazi wanakabwa koo vijijini kuchangia ujenzi wa madarasa.

Baadhi ya wazazi pia wameanza minong’ono kuwa watoto wao wamepewa mikopo kidogo, yaani Sh 600,000 kama ada vyuoni.

Hawajui kuwa miaka yote imekuwa hivyo na wakati mwingine wengi wanakuwa hawapati kabisa hata senti tano ya mkopo.

Sitanii, naomba nizungumzie kwa ufupi miezi sita ya Rais Samia akiwa Rais wa Tanzania baada ya kuapishwa Machi 19, 2021.

Nakumbuka vema kilichotokea, maana baada ya kifo cha Rais John Magufuli kulitokea kama sintofahamu hivi.
Wapo watu walioamini Rais Samia angeendelea kuwa Kaimu Rais, baadhi walidhani tunakwenda kwenye uchaguzi mpya na wengine hawakufahamu nini kitatokea.

Asubuhi ya Machi 18, 2021 niliamkia studio za Televisheni ya Taifa (TBC1) na TBC Taifa (radio) kufanya mahojiano na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk. Ayub Rioba.

Hii ilikuwa ni baada ya kifo cha Rais John Magufuli, kilichotokea Machi 17, 2021. Ikumbukwe wiki moja kabla nilikuwa nimefanya mahojiano na kituo cha Star TV nikasema tuambiwe bayana Rais Magufuli yuko wapi na anafanya nini.

Machi 18 pamoja na kwamba nilikuwa bado Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), ambapo baadaye nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa TEF Mei 22, 2021, ilinilazimu kutoa ufafanuzi huo uliokuwa tamko zito.

Sitanii, tamko nililolitoa lilizaa kuapishwa kwa Rais Samia kuwa Rais wa Awamu ya Sita Machi 19, 2021. Nilirejea Katiba ya Tanzania (1977) Ibara ya 37(5) inayosema: “Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uchaguzi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano na kwa masharti yaliyoelezwa katika ibara ya 40, kisha baada ya kushauriana na chama cha siasa anachotoka Rais atapendekeza jina la mtu atakayekuwa Makamu wa Rais na uteuzi huo utathibitishwa na Bunge kwa kura zisizopungua asilimia hamsini ya wabunge wote.”

Kwa mara ya kwanza kupitia makala hii ninakisema kilichotokea baada ya tamko hilo. Walinipigia simu watu wengi wakiwa na hofu.

Baadhi hawakufahamu Katiba inasemaje. Walinishutumu wakidai nimetangaza utaratibu wa kwangu, kwani baada ya kifo cha Rais kinachofuata ni uchaguzi.

Hii ilinipa shida kuona hata baadhi ya wabunge hawakufahamu nini kinafuata baada ya kifo hicho. Machi 18, 2021 itabaki kuwa siku ya kihistoria kwangu, kwani ujumbe nilioutoa ulitangazwa katika radio zote za ndani na za kimataifa na siku moja baadaye Rais Samia akaapishwa.

Sitanii, leo ninazungumzia mzigo wa madeni ambao Rais Magufuli amelitwisha taifa letu. Nimetangulia kusema na ninarudia, mimi ni msema kweli. Wala sipepesi macho katika kusema ukweli.

Wakati Rais Magufuli kwa miaka mitano yote alikuwa anawaaminisha Watanzania kuwa nchi inajenga miundombinu na inanunua ndege kwa kutumia fedha zetu wenyewe, uhalisia ni kinyume chake.

Kwa kipindi cha miaka mitano tu, Rais Mafuguli amekopa fedha nyingi kuliko fedha zote alizokopa Rais Benjamin Mkapa kwa miaka 10 aliyokaa madarakani.

Kwa miaka mitano, amekopa pia fedha nyingi kuliko alizokopa Rais Jakaya Kikwete kwa miaka 10 naye aliyokaa madarakani.

Rais Mkapa alirithi madeni mengi mno. Alipambana nayo, akaiingiza nchi katika Mpango wa Kusamehe Madeni Nchi Maskini (HIPC) na hadi anatoka madarakani, Tanzania ilikuwa inadaiwa Sh trilioni 20 tu.

Rais Kikwete wakati wake deni la taifa liliongezeka kwa Sh trilioni 23, hivyo akatoka madarakani deni la taifa likiwa Sh trilioni 43 kwa miaka 10. Rais Magufuli kwa miaka mitano tu, deni la taifa limeongezeka kwa Sh trilioni 29 na kufikia Sh trilioni 72 hadi anafariki dunia Machi, 2021.

Sitanii, kwa kasi hii ya ukopaji ina maana kama angekaa madarakani kwa miaka 10 kamili na akaendelea na kasi ya ukopaji wa wastani wa Sh trilioni 29 kwa miaka mitano, basi angetoka madarakani deni la taifa likiwa Sh trilioni 101 kufikia mwaka 2025.

Kuna jambo baya halisemwi. Rais Magufuli amekopa mikopo ya kibiashara inayoanza kulipwa baada ya miaka mitatu na inapaswa kulipwa ndani ya miaka minane, ikiwa na riba za kati ya asilimia 6 na 8.

Baadhi ya mikopo hii imeiva tayari. Imeanza kukuza deni la taifa kwa kasi kutokana na riba. Deni la taifa sasa limefikia Sh trilioni 78.

Kwa vyovyote vile iwavyo, Rais Samia anapaswa kuchukua hatua za haraka, ikiwamo kuunda timu ya majadiliano na wakopeshaji kwa ajili ya kubadili masharti ya mikopo ya kibiashara aliyochukua Rais Magufuli.

Anapaswa kuomba msamaha wa riba na pengine kuomba kuongezewa muda wa kulipa deni kama ulivyo utaratibu wa mikopo kwa serikali nyingi duniani.

Mikopo mingi kwa serikali huwa inalipwa kati ya miaka 20 hadi 50 kulingana na ukubwa wa mkopo na hutozwa riba kati ya asilimia 0.3 hadi asilimia 1. Mikopo ya aina hii inapatikana katika Benki ya Dunia, Shirika la Maendeleo Duniani, Benki ya Maendeleo Afika na nyingine za aina hii.

Kwa bahati mbaya na kwa masikitiko makubwa, kwa miaka mitano Wazungu tuliowaita mabeberu, ila tukawa tunakopa fedha zao kupitia benki za biashara. Kwa hali halisi, madeni haya yakiiva yote, ikiwa hakuna majadiliano ya dharura kuomba marekebisho ya masharti ya mikopo tuliyochukua chini ya Rais Magufuli, itafika mahala asilimia 60 ya bajeti ya taifa letu itakuwa inakwenda kulipa madeni. Waliomo serikalini watajua la kufanya katika hili.

Sitanii, ninafahamu baadhi ya wasomaji watakuwa wanaanza kufuka moshi kwa kusema ukweli huu. Wanajiuliza taarifa hizi nimezipata wapi? Taarifa hizi si za siri. Ziko wazi kwenye tovuti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Nimepitia taarifa za mapitio ya mwenendo wa uchumi tangu mwaka 2000 hadi 2021. Zipo mtandaoni na zinaonyesha deni lilivyokua hatua kwa hatua. Kwa nia ya kuweka uelewa unaofanana, ifuatayo ni hali ya deni la taifa tangu mwaka 2005 hadi 2021.

Oktoba 2005, deni la nje lilikuwa USD milioni 8,361.9 sawa na Sh 19,286,471,493,000 na deni la ndani lilikuwa Sh 1,712,800,000,000. Jumla kuu ya deni wakati Rais Mkapa anaondoka madarakani lilikuwa Sh 20,999,271,493,000 (Sh trilioni 20.9). Nimekokotoa hesabu hizi kwa kutumia viwango vya BoT vya kuuza dola ya Marekani ambavyo ni USD 1 kwa Sh 2,306.47.

Oktoba 2015, wakati Rais Kikwete anatoka madarakani deni la nje lilikuwa USD milioni 15,321.3, sawa na Sh 35,338,118,811,000 na deni la ndani lilikuwa Sh 7,826,200,000,000. Jumla kuu deni la nje na deni la ndani lilikuwa ni Sh 43,164,318,811,000 (Sh trilioni 43.1).

Deni la taifa lilianza kupanda kwa kasi Oktoba 2016. Deni la nje lilipanda na kuwa USD milioni 16,407.6 sawa na Sh 37,843,637,172,000, huku deni la ndani nalo likipanda na kuwa Sh 10,089,000,000,000. Jumla kuu ya deni ikafikia Sh 47,932,637,172,000 (Sh trilioni 47.9).

Oktoba 2017 deni la nje lilipanda kwa kasi kubwa na kufikia USD milioni 19,074.4 sawa na Sh 43,994,531,368,000. Kutokana na makandarasi kutolipwa deni la ndani nalo lilikua na kufikia Sh 12,563,300,000,000. Jumla kuu ya deni kwa mwaka huo likawa Sh 56,557,831,368,000 (Sh trilioni 56.5).

Oktoba 2018, deni la nje lilizidi kupanda na kuwa USD milioni 20,759.1 sawa na Sh 47,880,241,377,000, huku deni la ndani nalo likipanda na kuwa Sh 14,116,100,000,000. Jumla kuu ikawa Sh 61,996,341,377,000 (Sh trilioni 61.9).

Oktoba 2019, mwanamume aliongeza tena deni la taifa, deni la nje likafikia USD milioni 22,569.4, sawa na Sh 52,055,644,018,000, huku deni la ndani likipanda na kufikia Sh 14,187,400,000,000. Jumla kuu ya deni ikafikia Sh 66,243,044,018,000 (Sh trilioni 66.2).

Oktoba 2020, deni la nje lilipanda na kufikia USD milioni 23,599.3, sawa na Sh 54,431,077,471,000, huku deni la ndani likifikia Sh 15,608,500,000,000. Jumla kuu ikafikia Sh 70,039,577,471,000 (Sh trilioni 70).

Machi, 2021 wakati Rais Magufuli anafariki dunia, deni la nje la Tanzania lilikuwa limefikia USD milioni 24,429.2, sawa na Sh 56,345,216,924,000. Deni la ndani nalo lilipanda na kufikia Sh 16,116,500,000,000. Jumla kuu, deni la taifa lilifikia 72,461,716,924,000 (Sh trilioni 72.4).

Kilichofuata baada ya hapo, madeni yameanza kuiva kwa ajili ya kulipwa, huku mengine yakizalisha riba ya kufa mtu.

Makandarasi wengi Tanzania wanadai mabilioni kati ya hizo Sh trilioni 16 ambazo ni deni la ndani hawajalipwa siku nyingi. Kutokana na hali hiyo, madeni haya yaliyokopwa bila mpangilio katika benki za biashara yameanza kuwa msalaba kwa Rais Samia.

Taarifa ya hali ya Uchumi ya BoT ya Septemba, 2021 inayorejea mwezi Agosti, 2021 kutokana na mazingira hayo, deni la nje limekua na kufikia USD milioni 25,956.1 sawa na Sh 59,866,965,967,000, huku deni la ndani nalo likikua na kufikia Sh 18,225,000,000,000. Ukuaji huu unafanya kiwango cha deni la taifa kufikia jumla kuu ya Sh 78,091,965,967,000 (trilioni 78).

Sitanii, deni hili likigawanywa kwa Watanzania milioni 60, bila kujali mkubwa na mdogo, kila Mtanzania anadaiwa Sh 1,301,533 (Sh milioni 1.3). Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wanasema deni hili si tishio kwa uchumi wa taifa letu kwa sasa kwani liko katika uwiano wa asilimia 30 kwa uchumi wa taifa letu, wakati kuna mataifa Afrika ambayo tayari yana uwiano wa asilimia 54 ya deni kwa uchumi wa nchi zao, ila wanaionya serikali iepuke mikopo ya kibiashara ina riba kubwa, masharti mabaya na inalipwa kwa muda mfupi.

Pale Dodoma, tumeona Rais Samia ameanzisha utaratibu mpya wa ukweli na uwazi katika mikopo. Ameeleza fedha alizokopa zitafanya nini kwa kuorodhesha miradi itakayotekelezwa na akatueleza amezikopa kutoka wapi.

Ninajiuliza, hivi ilikuwa ni kwa faida ya nani Rais Magufuli na wapambe wake kuficha ukweli kuwa miradi ya reli, barabara, umeme, ujenzi wa hospitali na mingine mingi aliyoijenga alikuwa anakopa?

Hivi sisi kama tungejua anakopa, tungemzuia? Lakini si tungepata fursa ya kumshauri asichukue mikopo ya kibiashara inayoanza kututoa utumbo sasa? Mungu ibariki Tanzania.

Copyright ©2021. Gazeti la Jamhuri