Categories
Siasa

Chadema Inapokea Ruzuku Sh Milioni 109 Kwa Mwezi, Ni Kutokana Na “Halima Mdee Na Wenzake” Na Mbunge Kenani

Miezi miwili baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, vyama sita vyenye sifa ya kupata ruzuku vimeanza kuneemeka baada ya kuingiziwa mgawo wa fedha na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Vyama ambavyo vimevuna fedha hizo za mgao wa ruzuku hiyo unaotokana na idadi ya wabunge, madiwani na kura za urais ni pamoja na CCM, Chadema, ACT-Wazalendo, CUF, NCCR-Mageuzi na kile cha Democratic Party.

Kwa mujibu taarifa ambazo gazeti hili linazo, chama kinachoongoza kwa kuzoa ruzuku hiyo ni CCM yenye wabunge 354 ambacho kimepata zaidi ya Sh1.33 bilioni, Chadema ‘inayohesabiwa’ kuwa na wabunge 20 imepata Sh109.68 milioni, ACT Wazalendo yenye wanne kimepata Sh14 milioni na CUF yenye mbunge mmoja ikipata Sh5.7 milioni.

Vyama vingine vinavyopata ruzuku kwa idadi ya kura za madiwani ni pamoja na NCCR Mageuzi kilichoambulia Sh316,937, huku DP ikiambulia Sh63,387.

Chanzo: Mwananchi