Categories
Habari Siasa

ACT-Wazalendo Yatafakari Kujiunga Na Serikali Ya Umoja Wa Kitaifa Zanzibar

Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kinajipa muda zaidi wa kutafakari iwapo itapendekeza jina la makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar pamoja na kushiriki katika Serikali ya Umoja ya Kitaifa (SUK).

Akizungumza na gazeti la mwananchi lililotaka kujua msimamo wa chama hicho kuhusu ushiriki wake katika serikali ya umoja wa kitaifa kutokana na msimamo wake wa awali kutotambua Uchaguzi Mkuu uliopita na matokeo yake Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif amesema kuna haja ya kutafakari

“Kamati kuu (ya ACT-Wazalendo iliamua tusikubaliane katika siku saba kwasababu kuna mambo yanahitaji tafakuri ya kina na pia ni vizuri kushirikisha wanachama wetu” alisema Maalimu.

Kwa mujibu wa Ibara ya 39 ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010, Rais wa Zanzibar atamteua Makamu wa Kwanza wa Rais mwenye sifa za kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na atateuliwa na Rais baada ya kushauriana na chama kilichotokea nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya Uchaguzi wa Rais.

Hata hivyo, chama kilichotokea nafasi ya pili katika uchaguzi kinatakiwa kiwe kimepata si chini ya asilimia 10 ya kura zote.