Categories
Michezo/Burudani

Wataalam wa HR/Uajiri: Bodi Ya Simba Haijakiuka Taratibu Kumteua CEO Mpya Barbara Gonzalez

Kufuatia mjadala uliojitokeza jana baada ya Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba ya Tanzania kutangaza kuwa imemteua Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez, kuwa Afisa Mtendaji Mkuu kamili, gazeti la Habari Tanzania lilifanya mawasiliano na wataalamu wa masuala ya raslimali watu (human resources) na uajiri ili kupata mtazamo wao wa kitaalamu.

Kwa mujibu wa wataalam wote watatu waliohojiwa, kilichofanywa na bodi ya Simba ni kitu kinachofahamika kwenye masuala ya HR/Uajiri kama “direct appointment,’ ambapo kwa upande mmoja, mwajiri halazimiki kutangaza nafasi ya kazi husika, na kwa upande mwingine, anaweza kumteua mtu yeyote mwenye sifa stahili kushika wadhifa bila kutangaza mchakato wa kujaza nafasi hiyo.

Kwa kurejea kilichotokea kwenye klabu ya Simba, wataalam hao walieleza kwamba sio tu wanaamini kuwa Bodi ya klabu hiyo ina mamlaka ya kufanya “direct appointments,” kama zilivyo bodi za taasisi mbalimbali, bali pia kumteua Barbara, aliyekuwa akikauimu nafasi ya CEO, kushika wadhifa kamili ni jambo la kutarajiwa kutegemea utendaji kazi wake.

Barbara Gonzalez (@bvrbvra) | Twitter

Kuhusu “mwingiliano wa maslahi,” kwa vile Barbara pia ni msaidizi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed “Mo” Dewji, wataalam hao wote walisema hawaoni muingiliano wowote wa maslahi kwa sababu, Barbara kuwa msaidizi wa Mo hakumzuwii kutekeleza majukumu yake kama CEO kamili wa klabu hiyo. Na ushahidi katika hilo unaweza kuwa kwenye jinsi alivyomudu kukaimu nafasi hiyo baada ya kuondoka kwa mtangulizi wake, Senzo Masingiza, aliyeacha kazi na kujiunga na mahasimu wa Simba, Yanga.

Kuhusu uzoefu wa mwanamama huyo katika uongozi wa soka, wataalamu hao walikuwa na mwafaka kuwa nafasi ya CEO wa klabu ya soka inahitaji zaidi uzoefu katika menejimenti na uognozi kwa ujumla kuliko uzoefu wa soka, kwa sababu majukumu ya CEO ni ya kiutawala zaidi ilhali ya soka ni ya kiufundi na yapo mikononi mwa kocha mkuu na timu yake.

Mmoja wa wataalam hao alikwenda mbali zaidi na kupongeza hatua hiyo ya Bodi ya Wakurugenzi wa klabu ya Simba kwa kuweka historia nchini Tanzania, na nchi nyingi duniani, kwa kumteua mwanamke kushika nafasi hiyo muhimu katika uendeshaji wa klabu.