Categories
Michezo/Burudani

Messi Aomba Kuhama Barca

Lionel Messi looking dejected during Barcelona's Champions League defeat by Bayern Munich

Mwanasoka bora kabisa duniani wa klabu ya Barcelona ya Hispania, Lionel Messi, amewasilisha maombi ya kuhama timu hiyo. Messi, raia wa Argentina mwenye miaka 33 aliwasilisha ombi hilo leo Jumanne kwa njia ya fax akitumia kifungu kwenye mkataba wake kinachomruhusu kukatisha mkataba ghafla.

Wiki iliyopita, klabu hiyo ya Messi ilipata kipigo cha kihistoria baada ya kubugizwa goli 8 kwa mbili na mabingwa wa soka wa Ujerumani, Bayern Munich, katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Nguli huyo wa kabumbu alijiunga na Barcelona mwaka 2004 na ameshuhudia klabu hiyo maarufu kabisa duniani ikishinda Ligi ya Mabingwa wa Ulaya mara nne.

Bodi ya klabu hiyo itakutana hivi karibuni kujadili suala hilo, na inadhaniwa kujiuzu kwa rais wa klabu hiyo, Josep Maria Bartomeu, na uchaguzi wa mrithi wake mapema, vinaweza kumshawishi Messi abaki. Hata hivyo, mwanasoka huyo ameweka bayana msimamo wake kuwa anataka kuondoka.

Hali hiyo inatishia mvutano mkali wa kisheria kwani japo kuna kifungu kwenye mkataba wa Messi kinachomruhusu kuhama ghafla, anapaswa kutoa taarifa kabla ya Juni 10, tarehe ambayo imeshapita. Hata hivyo, Messi na wasaidizi wake wanadai tarehe hiyo inapaswa kusogezwa mbele kutokana na janga kurona kulazimisha msimu wa ligi wa nchi hiyo kusogezwa mbele.