Categories
Habari

“Zanzibar Ina Mashoga 3,600 na Makahaba 5,554,” – Waziri

UNGUJA imetejwa kuwa inaongoza kuwa na idadi kubwa ya wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili yao pamoja na wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja ikilinganishwa na Pemba.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Zanzibar, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Dk. Saada Salum Mkuya, alisema jumla ya wanawake 5,554 wanauza miili yao Zanzibar ambapo Unguja ni 4,854 na Pemba ni 700.

Alisema idadi ya wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja Zanzibar ni 3,300 ambapo Unguja ni 3,300 wakati Pemba ni 300.

Alisema asilimia kubwa ya maambukizo ya Virusi vya Ukimwi yapo kwa makundi maalum yakiwamo wanawake wanaofanya biashara ya miili yao ambayo ni asilimia 12, wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja asilimia 5 na wanaotumia dawa za kulevya kwa kujidunga sindano asilimia 5.1.

Alieleza takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya Zanzibar mwaka 2018 ambapo watu 2,600 Zanzibar wanatumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano Unguja ni 2,200 na Pemba ni 400.

Alisema wizara yake imeendelea na jitihada za kuyafikia makundi hayo maalum kwa lengo la kuyapa elimu na kupima maambukizio ya VVU na hadi kufikia Septemba mwaka huu, jumla ya watu 10,378 wa makundi maalum wamefikiwa na 6,424 walikubali kupima VVU ambapo 69 waligundulika na maambukizi ya VVU.

Waziri huyo alieleza kuwa kutoka Julai mwaka jana hadi Juni mwaka huu, jumla ya wajawazito 56,165 wamefanyiwa uchunguzi wa VVU ambapo kati yao 104 waligundulika na VVU, watoto 381 waliozaliwa walichunguzwa afya zao na watano waligundulika na maambukizi ya virusi hivyo.

“Katika kudhibiti maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kiwango cha maambukizi chini ya asilimia tano kinachukuliwa kama ni ishara ya ufanisi katika kuwalinda watoto dhidi ya maambukizi kutoka kwa mama zao,” alisema Dk. Saada.

Alieleza katika kuibua mbinu za kudhibiti mazingira hatarishi yanayoweza kuchangia kuongezeka kwa maambukizi ya VVU, wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, imeweka utaratibu kudhibiti upigaji wa ngoma na muziki katika maeneo mbalimbali Unguja na Pemba kwa kuzuia vibali.

Alisema pia wamefungia baa na nyumba za kulala wageni na hoteli zinazoendeshwa kinyume cha utaratibu au zinazochochea tabia hatarishi pamoja na kudhibiti bandari zisizorasmi kwa kusimamia uingiaji wa wageni wasiokuwa na shughuli zinazoeleweka.

Aidha, alisema Zanzibar bado inakabiliwa na tatizo la unyanyapaa kwa wanaoishi na VVU, licha ya elimu inayotolewa kwa jamii, hivyo aliwasisitiza wananchi kuacha unyanyapaa