Categories
Habari

ZAIDI ya watu 4,000 wameng’atwa na mbwa katika kipindi cha mwaka mmoja wilayani Moshi

 

ZAIDI ya watu 4,000 wameng’atwa na mbwa katika kipindi cha mwaka mmoja wilayani Moshi huku wafugaji wa wanyama hao wakitakiwa kuwapa chanjo kabla ya utaratibu wa kuwaua haujaanza.

Aidha imebainika asilimia kubwa ya wanaong’atwa na mbwa hao ni wanafunzi nyakati za asubuhi wanapokwenda shule, hivyo kuongeza hofu ya kuibuka kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Mganga wa Mifugo Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Dk Walter Marandu alisema hayo katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Yamu Makaa, kata ya Kirua Vunjo Kusini wilayani hapa.

Akizungumza kwa niaba mganga huyo, Ofisa Mifugo kata ya Kirua Vunjo Kusini, Esther Faniki alisema serikali inaandaa mpango wa kuwafikisha mahakamani wananchi watakaokaidi kufungia wanyama hao na wasiowapa chanjo.

Dk Marandu alisema hadi sasa hakuna mwananchi aliyepata ugonjwa wa kichaa cha mbwa na kwamba wapo zaidi ya mbwa 8,000 wilayani hapa ambapo halmashauri inatarajia kuwauwa zaidi ya 200.

Alitaja maeneo yaliyokithiri kwa uwepo wa mbwa hao ni Njia Panda ya Himo, Makuyuni na Kahe wilayani hapa ambapo maafisa wa serikali wataandaa utaratibu wa kuwaua kwa sumu ama kuwapiga risasi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Yamu Makaa, Omary Mdee alisema mbwa ni kero kwani pamoja na kung’ata watu lakini pia wanakula mbuzi na kuku na kusababisha migogoro baina ya wananchi wenyewe kwa wenyewe.