Categories
Habari

Wimbi La Vijana Watumia Ugoro Waongezeka Nchini

Katika kipindi cha hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la vijana wanaotumia ugoro kama kilevi ikilinganishwa na miaka ya nyuma ilikozoeleka kama starehe ya wazee.

Mwananchi limepita maeneo mbalimbali ya Mji wa Moshi kuzungumza na baadhi ya watumiaji na wauzaji wa ugoro kujua siri iliyopo katika bidhaa hiyo ambayo imewavutia vijana kuanza kuitumia kama kilevi.

Ugoro ni tumbaku iliyosagwa na watumiaji wake huvuta puani unga huo, wengine huilamba.

Kelvin John, mkazi wa Moshi anayefanya kazi ya upagazi Mlima Kilimanjaro, ni mmoja wa vijana wanaotumia ugoro. Anasema amekuwa akiutumia kama mbadala wa sigara.

Anasema awali alikuwa akivuta sigara lakini kutokana na kazi yake ya upagazi alilazimika kuacha na kuhamia kwenye ugoro.

“Nilikuwa mvutaji mkubwa wa sigara na kwa siku nilivuta zaidi ya pakiti mbili, lakini mazingira ya kazi yangu kama mpagazi katika Mlima Kilimanjaro nililazimika kuacha sigara maana haturuhusiwi kuvuta tukiwa mlimani, hivyo nikatafuta njia mbadala ya kuisahau sigara,” anasema.


Anasema aliamua kujifunza kuvuta ugoro na baada ya muda aliuzoea na kumfanya aisahau kabisa sigara kwa kuwa kilevi au raha aliyokuwa akiipata kwa kuvuta sigara kwa sasa anaipata katika ugoro kwa kiwango kikubwa zaidi.

“Ugoro kwangu ni mbadala wa sigara na nikitumia inanipa raha kama vile nimevuta sigara yaani napata mzuka zaidi ya ule niliokuwa naupata kwenye sigara maana ugoro ni zaidi na nikiutumia napata ujasiri wa kufanya lolote,” anaongeza.

Anaeleza ugoro anaweza kwenda nao hadi mlimani hawazuiwi na kichupa hawezi kukitupa mlimani kuharibu mazingira, ni lazima muda wote akiweke mfukoni hata kama ugoro utakuwa umeisha ili baadaye akirudi mjini aweke mwingine.

“Yaani ugoro ni kilevi kizuri na mtu anaweza kuutumia kuvuta au kula na akalewa kabisa kama vile amekunywa pombe,” anasema Kelvin.

Naye Lazaro Shabaan anaeleza kuwa ugoro ni kilevi cha bei rahisi na anaweza kuutumia mahali popote bila hofu kwa kuwa siyo kilevi haramu.

“Ugoro ni bidhaa ya bei nafuu, unanipa stimu ya haraka lakini naweza kuingia nao popote na ninaweza kuutumia mahali popote bila hofu wala kuwabugudhi watu tofauti na sigara ambayo nikiwa mahali na watu, nalazimika kutoka kwenda pembeni kuvuta nimalize ndipo nirudi,” anasema.

Lazaro anasema bei ya ugoro, ambao mara nyingi huuzwa kwenye vifungashio huanzia Sh200.

Wafanyabiashara wafunguka

Baadhi ya wafanyabiashara wa ugoro katika Soko Kuu mjini Moshi wanasema ni biashara nzuri na wateja wao wakubwa kwa sasa ni vijana.

Anna Joshua, anasema zaidi ya asilimia 97 ya wateja wake wa ugoro ni vijana ambapo ndoo moja ya lita 20 hununuliwa kwa Sh60,000.

Anasema kwa miaka ya nyuma, wateja wa ugoro walikuwa wazee na baadhi ya vijana wa kabila la Kimasai lakini kwa sasa watumiaji wengi ni vijana na wa rika na kada mbalimbali.

“Kisado (ndoo ndogo) hiki kimoja cha ugoro, nakinunua kwa Sh60,000 lakini huwa nafunga wa Sh200 na baada ya kuviuza vyote napata Sh80,000 hivyo kwa ndoo mmoja ndogo naweza kupata faida ya zaidi ya Sh20,000 na kwa siku naweza kuuza hata zaidi ya ndoo mbili ndogo, inategemeana na siku,” anasema Anna.

Naye Fatuma Iddi anasema kwa sasa bidhaa hiyo imekuwa ikichangamkiwa sana na vijana tofauti na zamani kama ilivyozoeleka kwa kuwa ni kilevi kinacholewesha haraka kuliko pombe

“Siri kubwa iliyofanya vijana kutumia ugoro ni kilevi kinacholewesha haraka, kwani mtu akitumia cha Sh200 tu, analewa.

“Ukiwa na ugoro mzuri, akija kijana mmoja kuuonja, unasikia anakwambia huu uko vizuri mambo ni moto, akiondoka baada ya muda unawaona wengine wamekuja kuuchangamkia hadi unaisha na wanaposema ni mzuri maana yake ni kuwa kilevi chake kiko vizuri,” anasema Fatma.

Anasema bidhaa hiyo kwa bei ya jumla anauza pakiti moja kwa Sh100 huku bei ya rejareja akiuza kwa Sh200 kwa pakiti.

“Kwa kweli biashara hii ni nzuri kwani mimi hapa nafunga vifurushi vingi na kumaliza, ikitegemeana na siku na ladha ya ugoro nilio nao na kwa ndoo moja ndogo naweza kupata faida ya hata Sh20,000.

“Mfano ugoro ninaouza Sh2,000 kwa bei ya jumla, anayeenda kuuza kwa bei ya rejareja anapata Sh4,00, ukiangalia hapa ni kwamba anapata faida nzuri sana, sasa hiyo maana yake bidhaa inatoka kwa kuwa ina wateja wengi,” anasema.Daktari azungumza

Wakati bidhaa hiyo ikiendelea kujipatia umaarufu na kutumiwa zaidi na vijana, wataalamu wa afya wanatahadharisha kuwa una madhara mbalimbali kiafya kwa watumiaji.

Dk Kareem Segumba, ambaye ni mhadhiri mwandamizi wa Chuo Cha Sayansi ya Tiba Zanzibar, anaeleza kuwa ugoro upo kwenye makundi ya dawa za kulevya na kwamba ndani yake kuna michanganyiko tofauti ambayo husababisha athari za kiafya.

“Ndani ya ugoro kuna kemikali nyingi ambayo baadaye huleta madhara kiafya, kemikali hizo ni kama vile, nicotine, nitrosamines na nyinginezo,” anasema Dk Segumba.

Anaeleza kuwa matumizi ya ugoro yanayochangamkiwa na vijana hata watu wazima yamegawanyika sehemu mbili. Anasema wapo wanaouvuta puani na wengine huuweka ugoro mdomoni, chini ya fizi.

“Ugoro una kilevi ndani yake kutokana na kuwepo kwa hizo kemikali, hivyo mtu atumiapo ugoro siyo rahisi kuacha,” anasema Dk Segumba.

Anasema madhara makubwa ya kiafya yaletwayo na matumizi ya ugoro, mara nyingi huonekana baada ya matumizi ya muda mrefu.

“Kwa kuwa kemikali zinazopatikana kwenye ugoro zina visababishi vya saratani kuna uwezekano wa sehemu mbalimbali za viungo vya mwili kuathirika kutokana na sumu zilizokuwamo kwenye ugoro.

“Utafiti umefanyika kwenye vyuo vikuu hasa vya nchi za Norway na Denmark umeonyesha ugoro una uwezo mkubwa wa kuleta saratani mwilini na viungo ambavyo vipo kwenye athari ya kupata saratani ni fizi, ulimi, kinywa, kongosho, koromelo na tumbo” anaeleza Dk Segumba.

Dk Segumba anaongeza kuwa madhara ya mengine ya ugoro ni kuchubuka kwa midomo na fizi, kulegea na kutokwa meno ya mbele, meno kubadilika rangi na kuoza pamoja na kutoa harufu mbaya kinywani.

Aidha anasema madhara ya ugoro huanza kuonekana baada ya mtumiaji kuendelea kuwa mteja wa bidhaa hiyo kwa miaka mitano hadi 10 na kwamba ugoro wa kunusa unafanya mtumiaji awe na hatari ya kupata magonjwa ya viungo vya mfumo wa hewa.

Chanzo: Mwananchi