Categories
Habari

Tanzia: Mwandishi Nguli Wa Riwaya Za Kishushushu John le Carré Afariki.

Galacha wa uandishi wa riwaya za kishushushu, John le Carré amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89.

Mwandishi huyo Muingereza ambaye kifo chake kimetokana na homa ya mapafu (pneumonia) aling’ara kwenye fani ya uandishi riwaya za kishushushu kwa takriban miongo 6, huku kazi zake bora zaidi zikiwa ni pamoja na riwaya ya “The Spy Who Came in From the Cold” (iliyochapishwa mwaka 1963) na “Tinker Tailor Soldier Spy” (ya mwaka 1974).

Riwaya ya “Tinker Tailor Soldier Spy” ilipelekea kutengenezwa filamu maarufu iliyobeba jina hilo hilo

Baada ya anguko la ukomunisti mwanzoni mwa miaka ya 1990, mwandishi huyo aligeukia mabadiliko ya mazingira ya usalama duniani, na kuwapeleka “majasusi wake wa kufikirika” Israeli, Mashariki ya Kati, Afrika, Asia, na Amerika ya Kati katika riwaya kama “The Little Drummer Girl,”The Night Manager,” “The Tailor of Panama,” na “The Constant Gardener.”

Utunzi wa riwaya zake ilichangiwa na ukweli kwamba yeye mwenyewe aliwahi kuwa shushushu katika Idara ya ushushushu wa ndani ya Uingereza inayojulikana kama MI5 na ile ya ushushushu wa nje inayofahamika kama MI6.

Makao Makuu ya MI5, Milnbank, London
Makao Makuu ya MI6, Vauxhall, London

Na ni kutokana na kuwa shushushu ndio maana alilazimika kutumia jina “John le Carré” badala ya jina lake halisi, David Cornwell.