Categories
Habari

Sheikh Ponda Alaani Kukamatwa Kwa Askofu Mwamakula

SI SAWA KUMKAMATA ASKOFU KWA MADAI YA KATIBA MPYA

Kwa hakika hali inazidi kuwa ngumu kuelewa mwelekeo wa nchi yetu katika mambo mbalimbali.

Mfano mmojawapo ni huu wa vyombo vya Dola kumkamata kiongozi wa Dini Askofu Emmaus Mbandekile Mwamakula kwa kuleza nia yake njema katika suala la Katiba Mpya.

Askofu kasema suala analoliona ni kipaumbele cha taifa kwa sasa ni kurejea katika kiporo cha Katiba Mpya ya Tanzania.

Pili kaeleza nia yake ya kuwaunganisha wananchi katika kukumbusha mamlaka ya utekelezaji (serikali) kuhusu suala hilo.

Tatu kaeleza njia anayokusudia kuitumia kuunganisha hisia za wananchi ni matembezi ya amani.

Aidha kwakuwa sheria ya nchi inamtaka kutoa taarifa ya matembezi ya namna hiyo kwa vyombo vya usalama ndani ya masaa 24, kabla, na kwakuwa muda wa kufanya hivyo bado upo, kosa liko wap?

Au lipi ambalo ni kosa katika mambo hayo matatu. Yaani kuelekeza fikra za Watanzania katika Katiba Mpya ni kosa? Au kuikumbusha serikali umuhimu wa kuzindua mchakato wa Katiba Mpya? Au kuwaleta wananchi pamoja kwa matembezi ya amani?

Huko nyuma tulikua tunajua siasa yetu ni ya ujamaa na kujitegemea. Ingawa hatuisifu lakini tulikuwa tunaijuwa.

Hii siasa ya sasa ya wananchi kutotakiwa kusema fikra zao, kuhoji, kukumbusha wala kutumia haki zilizomo ndani ya Katiba ya nchi, ni siasa mpya na kwakuwa msingi wake haufahamiki, bilashaka inawaathiri wananchi kiakili, kielimu, kisiasa, kiuchumi, kimaendeleo na kuwaondolea furaha.

Msimamo wetu:

  1. Tunapinga tamko la kumdhalilisha kiongozi wa Dini lililotumiwa na vyombo vya Dola kwa kumwita “anayejiita Askofu”.
  2. Tunamtambua Askofu Mwamakula kama mmoja wa viogozi wa Kanisa la Moravian na wa Dini ya Kikristo Tanzania
  3. Tunaunga mkono vuguvugu la madai ya Katiba Mpya.
  4. Tunavikumbusha vyombo vya Dola haki ya msingi ya kumwacha huru kiongozi huyo. SHEIKH PONDA ISSA PONDA

Katibu Mkuu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania.