Categories
Habari

Mchungaji Ashikiliwa na TAKUKURU kwa “Mikopo Umiza” Yenye Riba Hadi 200%

Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Kiinjilisti la Kilutheri Tanzania wilayani Babati, Emmanuel Petro Guse, anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuwia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kuendesha biashara ya mikopo umiza bila ya kuwa na leseni ya biashara ya ukopeshaji fedha.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara Holle Joseph Makungu akizungumza mjini Babati Agosti 28 amesema awali walipata malalamiko toka kwa mkazi wa Bashnet aliyekopa sh200,000 na kurejesha sh 400,000.

Makungu amesema mchungaji huyo baada ya kupewa sh400,000 akawa anadaiwa sh480,000 kutokana na mkopo huo hivyo TAKUKURU wakamuita mchungaji Guse kwa mahojiano.

Amesema baada ya mchungaji huyo kuitwa na TAKUKURU aligoma kutii hivyo wakatumwa makachero waliomkamata kisha kumuhoji endapo anaendesha biashara ya kukopesha ila akakana.

Amesema ilibidi makachero hao wafanye upekuzi nyumbani na ofisini kwa mchungaji huyo na kupata mikataba ya mikopo umiza 48 ikiwa nyumbani kwake.

“Baada ya kukuta nyaraka hizo makachero wetu walimchukua mchungaji huyo hadi ofisini kwetu na kufanya naye mahojiano kisha akakiri kufanya biashara ya mikopo umiza bila kuwa na leseni,” amesema Makungu.

Amesema mtuhumiwa huyo alihojiwa juu ya mlalamikaji huyo kukopa sh200,000 kisha kulipa sh400,000 na bado anadaiwa sh480,000 alikiri hilo.

“Mchungaji huyo bado anashikiliwa na TAKUKURU kwa uchunguzi wa mikataba umiza 48 aliyokutwa nayo nyumbani kwake wakati wa upekuzi,” amesema Makungu.

Ametoa wito kwa wananchi wa maeneo ya Bashnet, Ufana, Madunga na vijiji vinavyozunguka eneo hilo kufika kwenye ofisi za TAKUKURU kuanzia Agosti 29 ili changamoto zao ziweze kushughulikiwa kwa pamoja.

Ametoa rai kwa wanachama wa Manyara, kutokubali kulipa riba hizo kubwa kwa wakopeshaji ambao hawana leseni na hawalipi kodi serikali kwani biashara hiyo ni haramu na kinyume cha sheria, watoe taarifa TAKUKURU ili wakopeshaji hao waweze kukamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.