Categories
Habari Uchumi

Mbunge Mpina Awashangaa Wabunge Kupiga Makofi Kuhusu Sh Trilioni 1.3 Kutoka IMF Ilhali SHILINGI TRILIONI 360 ZILIZOPASWA KUKUSANYWA NA SERIKALI HAZIJULIKANI ZILIPO

MBUNGE wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina amehoji bungeni zilipo fedha za watanzania Shilingi Trilioni 360 ambazo Serikali ilipaswa kuzikusanya huku akishauri Mkataba baina ya Kampuni ya SICPA na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhusu Mtambo wa ETS uvunjwe kwani umelisababishia taifa hasara kubwa.

Mpina amesema hayo bungeni Dodoma wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2022/2023 pamoja na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2022/2023 huku akimpongeza Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyolipambania taifa na hotuba zake nzuri zenye msisimko mkubwa katika mikutano miwili ya kimataifa aliyohudhuria hivi karibuni.

Mpina amezungumzia namna Serikali inavyoshindwa kukusanya fedha nyingi kutokana na kutokuwepo usimamizi madhubuti akitolea mfano suala la rufaa za kikodi kutofanyiwa kazi zilizoigharimu Serikali kupoteza Trilioni 360 ambazo zingetumika kwenye shughuli za maendeleo ya wananchi.

“Mhe. Mwenyekiti tulisema hapa wabunge tunazo Trilioni 360 zimeshikiliwa na Mahakama, uamuzi haujatoka nilitegemea kwenye mpango hapa isemwe kwamba hizo Trilioni 360 ziko wapi leo hapa Bunge zima linapiga makofi kwa Trilioni 1.3 tulizopewa na IMF fedha ndogo Trilioni 1.3 tunapiga makofi mpaka mikono inauma na kwakweli tunashukuru kwa hilo,” amesema Mpina.

Mpina amesema asilimia 10 Trilioni 360 ni Trilioni 36 lakini bado hilo halijawauma, Bunge halijaumia, Serikali haijaumia lakini fedha zimeshikiliwa tu kinachosubiriwa ni maamuzi tu ya Mahakama.

“Kama tatizo ni hizo bodi zetu za rufaa za kodi zinashida ya wataalamu si tuajiri hata wataalamu wa kutoka nje kama tatizo ni wataalamu nini kinachosababisha mpango haujazungumza suala hilo?” amehoji Mpina.

Aidha Mpina amekumbishia suala la ‘transfer pricing’ ambalo wabunge walishauri Serikali wakati wa Bunge la Bajeti mwaka huu kwamba kuna makampuni ya kimataifa 504 yenye miamala zaidi ya Trilioni 105 kwa mwaka na uwezo wa TRA kuyakagua makampuni hayo ni asilimia 1, TRA haina wataalamu, haina fedha na haiwezi kukagua miamala hiyo ya TP na hivyo Serikali haiwezi kupata kodi katika maeneo hayo fedha nyingi za watanzania zinapotea.

“Mhe. Mwenyekiti haya yote kwetu sisi mipango yetu hatuoni kama ni shida lakini tukiletewa hata bilioni 5 tunafurahi kweli kweli lakini fedha zetu zimeshikiliwa na watu hatupati hasira katika hili” amehoji.

Aidha Mpina akashangaa kuona Mpango uliowasilishwa bungeni haukuongelea juu ya mikataba mibovu namna ilivyoshughulikiwa ukiwemo wa ule wa Kampuni ya SICPA na TRA kupitia Mtambo wa ETS.

“Mhe. Mwenyekiti nilitegemea hata mikabata mibovu ya kina SICPA na TRA ingezungumzwa humu kwamba tunaenda kuifuta mara moja, mikataba ya kinyonyaji ambayo inanyonya fedha za watanzania tungeweza kufuta mikataba kama hiyo tukapata mapato mengi tu ya Serikali” amesema Mpina.

Pia Mpina ametilia shaka uwezo wa Msajili wa Hazina katika kusimamia Mashirika ya Umma 237 yaliyoko nchini kwani yaliyo mengi yameshindwa kutekeleza majukumu yake na kugeuka kuwa mzigo kwa Serikali badala ya kujiendesha kwa faida na kutoa gawio kubwa serikalini.

“Mhe Mwenyekiti tunaye TR anasimamia Mashirika ya Umma 237 yamekuwa mzigo mkubwa kwa Serikali yanategemea ruzuku kutoka serikalini yameshindwa kuwezeshwa kupewa fedha hayana mtaji yapo tu hayatekelezi majukumu yake sawasawa lakini kwa nini mpango hauzungumzi juu ya mashirika yetu ya umma kuyapatia mtaji yaweze kufanya biashara tuweze kupata gawio kubwa la Serikali hela tunazozipeleka kwa ajili ya ruzuku zifanye mambo mengine lakini kwetu sisi tunaona hii ni sawa tu” Amesema Mpina.

Mpina amesema hadi sasa Msajili wa Hazina anauwezo wa kuyasimamia mashirika hayo kwa asilimia 13 tu lakini hana fedha, hana wataalamu lakini kwetu sisi tunaona kukaa na kupanga ni sawa lakini msingi wa matatizo haya yanayotukabili hatuufanyii kazi tatizo letu liko wapi?

Mpina pia ameukosoa vibali Mpango wa Maendeleo uliowasilishwa bungeni akitilia mashaka juu ya kutofanyika tafiti za kujua ni kwa namna gani Serikali inaweza kuboresha vyanzo vya mapato jambo linalosababisha kuwepo mgogoro mkubwa kwa wananchi akitolea mfano sakata la tozo za miamala ya simu.

“Kwa mfano hivi ni utafiti gani tunaoufanya kila mwaka kwanini huu mpango usituambie tunafanya utafiti gani kufikia ukusanyaji wa mapato yetu, vyanzo vyetu vya mapato tumevifanyia utafiti? Hao TRA wanapofanya ukusanyaji wa mapato tunawachunguza namna gani uwezo wao wa kuweza kukusanya mapato yetu na tunachukua hatua gani? sasa unakuta mwisho wa siku mnaingia kwenye bajeti mnasema tu hili limesamehewa hiki kimetozwa hili tozo tumeongeza na mfano upo”amesema Mpina.

Hata hivyo Mpina ametolea mfano kilichotokea hivi karibuni kuhusu tozo ni kwa sababu ya kutokuwa na utafiti wa kutosha katika mapato na kujikuta wakiingia kwenye mgogoro mkubwa sana na wananchi.

“Tumeingia kwenye mgogoro mkubwa kwenye tozo za simu tumebishana hapa tukatoka tulivyotoka tumefika mahala tukarekebisha wenyewe viwango vya tozo vya simu vilivyokuwa vikubwa vya miamala, tumeenda na withholding tax tukawaambia watu kwamba tunataka kuweka withholding tax kwenye mazao ya asilimia 2 halafu tukasema tukaenda kusamehe wanywa bia kwamba wasilipe kodi ili zao la shayiri liweze kuzalishwa,” amesema.

“Wakati huo unamsamehe mnywa bia ili kilimo kiongezeke halafu unaenda kumtoza anayelima shayiri yenyewe sasa unaenda kutoza withholding tax asilimia 2 huku ukijua una service levy asilimia 3 huyo mkulima atalimaje? matokeo yake najua watakuja kufanya marekebisho hapa,” amehoji.

Mpina pia akagusia suala la ongezeko la tozo kwenye mafuta nayo ilipigiwa kelele bungeni kuwa itakwenda kusababisha mfumko wa bei na kupanda gharama za maisha lakini ushauri huo haukusikilizwa.

“Tumekwenda kwenye mafuta na kwenyewe hivyo hivyo tulisema inaweza ku attract inflation hata kama tuna nia hiyo njema Serikali imefanya marekebisho katikati ya safari hii yote ni uthibitisho kwamba tunaibuka na mabadiliko ya kodi bila kufanya utafiti wowote na kwa nini hatufanyi utafiti, na kwanini hatuwekezi, na kwanini suala la hili la mapato limekuwa la siri siri tu siri siri tu halafu linakuja kuibuka hivi hakuna mafanikio ambayo tunaweza kufika nayo popote lakini mpango hauzungumzi,” amehoji Mpina.

Mbali na hayo Mhe. Mpina amehoji sababu ya mpango huo kutoonyesha mkakati wa udhibiti wa utoroshaji wa rasilimali za taifa ikiwemo madini, mazao ya uvuvi, mifugo, misitu, wananyama pori ambako mapato mengi ya Serikali yanapotea kutokana na usimamizi dhaifu.

“Mhe. Mwenyekiti bado tuna maeneo mengi kuna utoroshaji mkubwa sana wa fedha, ukienda mipakani mle madini yetu bado yanatoroshwa, mazao yetu ya uvuvi bado yanatoroshwa, mifugo yetu bado inatoroshwa, misitu na hata wanyama pori bado wanatoroshwa mpango unatueleza nini unaenda kudhibiti namna gani maeneo haya ili tuweze kupata mapato” amehoji Mpina.

Mpina amesema kwenye mpango huo unaonyesha kuwa mapato ya Serikali yataongezeka kwa trilioni 2.18 katika mwaka wafedha 2022/2023 lakini hakuna ulipoonyesha tunaweza kufikiaje mapato hayo.

“Mhe. Mwenyekiti ukiangalia hapa sasa hivi tunazungumza kwenye mpango huu kwa mwaka unaokuja wa fedha mapato yetu tunayotegemea kuongezeka ni Trilioni 2.18 peke yake lakini ukiangalia hiyo Trilioni 2. 18 wanaipata wapi na hilo ongezeko wanalipata wapi wanasema mapato yataongezeka kwa asilimia 7.6 lakini 7.6 wameipataje wakati uchumi utakua kwa asilimia 5.2,” amesema Mpina.

“Mfumko wa bei utafikia kwenye asilimia 4 tayari ni asilimia 9.2, bado kuna kuongezeka kwa tozo kuna kuja na kodi mpya ambayo walau asilimia 1 tunapata asilimia 10.2 bado kuna udhibiti wa upotevu wa mapato kama huu tunaozungumza tukishaweka mikakati kama hiyo nayo kuna kama asilimia 1 kwa hiyo unaweza ukakuta mapato yetu yangeweza kuongeweza kukua hata kwa asilimia 12,” amesema Mpina.

Mpina ameongeza kuwa kama wangekua wanafanya utafiti wa kutosha kuhusu mapato ni dhahiri utekelezaji wake ungekuwa mzuri na mapato mengi zaidi yangepatikana.

“Lakini hapa tunafika tunasema mapato yataongezeka kwa trilioni 2.18 alafu inatokana na nini kwa hiyo wakusanyaji nao wenyewe wanaenda kiuzembe kukusanya wanashindwa kushughulikia fedha hizi ambazo zipo za kuchukua tu kwa sababu sisi wabunge tumewaidhinishia makadirio madogo sasa Mhe. Mwenyekiti tutabaki hapa mpaka lini,” amehoji Mpina.

Kuhusu Sekta Binafsi, Mhe. Mpina amesema ni vigumu sekta hiyo kuweza kupiga hatua kubwa kama inaendelea kudhulumiwa kwa kiasi hicho kutokana na kutotendewa haki.

“Kuhusu ushiriki wa sekta binafsi hatuwezi kukua kama ushiriki wa sekta binafsi tunaenda nao namna hii kama sekta binafsi itaendelea kudhulumiwa namna hii, Mhe. Mwenyekiti Sekta Binafsi ambapo taarifa zetu za madeni watu wa sekta binafsi walikuwa wanatudai Trilioni 3.8 tulivyoanza uhakiki mwaka 2015/2016 , katika uhakiki huo madeni ya kiasi cha Tshs Trilion 1.16 hayakukidhi vigezo na hivyo sio madeni halali” amehoji Mpina.

Mpina amesema karibia asilimia 30 ya madeni hayo sio halali na anayesema ni Serikali sio wananchi waliokopwa na kwamba kitendo hicho ni dhuluma kwa wananchi.

“Wewe unakuja kuhakiki huku deni langu nilishakupa service ukapata Service hiyo halafu unakuja kusema hili deni zaidi ya asilimia 30 siyo halali, walioingia madeni hayo ni akina nani, waliruhusiwa na nani na wamechukuliwa hatua gani ambao walidanganya hilo mnaenda kuwaadhibu hawa wananchi ambao ni haki yao kumdhulumu mtu kwa fedha au kwa mali uliyoichukua ni sawa sawa na ujambazi mwingine tu kwa nini Serikali iingie kwenye ujambazi wa namna hiyo asante sana Mhe. Mwenyekiti,” amesema Mpina.

Aidha Mpina ameshauri ni muhimu michango na mawazo ya wabunge inapotelewa ifanyiwe kazi ili kuleta ustawi wa maendeleo ya taifa letu kwani umeibuka mtindo wa mawazo ya wabunge kutofanyiwa kazi na matokeo yake ni kusababisha matatizo mengi kwa wananchi.

“Mhe. Mwenyekiti mipango hii inafika mahala tunaweza kuwa tu kwenye mipango muda wote na hata yale tunayoyazungumza wakati mwingine yasipate muda wa kufanyiwa kazi,”

“Mhe. Mwenyekiti tulizungumza mengi sana wakati tunapitisha bajeti ya mwaka huu na mimi naamini kama yale tuliyoyazungumza wakati huo kama kuishauri Serikali kama yangezingatiwa kwenye huu mpango tuliowasilishiwa leo hii tusingekuwa na maneno mengi hivi ya kusema lakini niseme hayo tuliyoyazungumza na ushauri wote tuliousema hatuyaoni kwenye Mpango sasa tutashauri mpaka lini ili tuweze kusikilizwa” amehoji Mpina.

Pia Mpina amesema kupitia bunge hilo wabunge walishauri masuala mbalimbali ya maendeleo ya sekta binafsi, vijana na ukusanya mapato lakini kwenye mpango huo ushauri huo haukuzingatiwa.

“Tulishauri mengi sana kuhusu ajira za vijana wetu zinapatikanaje, tulishauri mengi sana kuhusu sekta binafsi, tulishauri mengi sana kuhusu mapato ya Serikali, tulishauri mengi sana kuhusu kumaliza umasikini Tanzania lakini Mhe. Mwenyekiti ukipitia mpango huoni ni wapi sasa ambako maoni yetu yamezingatiwa” amesema Mpina.