Categories
Habari

Askofu Mwamakula: Tunduma Hali Si Shwari

Anaandika Baba Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula – Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki

TUNDUMA HALI SIO SHWARI!

Hali ya Tunduma mkoani Songwe siyo nzuri. Hadi sasa wamekufa watu wawili mmoja wa CCM na mwingine wa CHADEMA. Vurugu zilizosababisha vifo hivyo zina uhusiano kwa sehemu na ‘mienendo’ au ‘matendo’ ya baadhi ya Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi kuhusiana na suala zima la kutenda haki katika mchakato wa Uteuzi wa Wagombea mkoani Songwe. Kwa upande mwingine ni mvutano kati ya CCM na CHADEMA wanaogombania umiliki wa Tunduma kisiasa!

Sisi kama viongozi wa dini tumeonya na tumeendelea kuonya sana juu ya mwenendo wa baadhi ya Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi katika Majimbo na Kata nchini kote. Kwamba malalamiko na hisia kutoka kwa baadhi ya vyama vya siasa kuonewa visiposhughulikiwa huondoa utulivu katika jamii. Tunduma sasa hali inaelekea mahali pabaya.

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Tunduma, Mheshimiwa Frank Mwakajoka amenieleza kwa mtazamo wake hali ilivyo kule. Anasema Wagombea Udiwani watatu wa CHADEMA wameunganishwa katika Kesi ya Mauaji. Anaendelea kueleza kuwa: “Kuna Madiwani wengine wanaotakiwa kukamatwa wakiwemo Ally Mwafongo (Kata ya Makambini), Mosses Mshani (Kata ya Muungano), Frowini Mwalongo (Kata ya Maporomoko), Osiah Kibwana (Kata ya Kaloleni), Boniphas Mwakabanje (Kata ya Majengo) na M/kiti wa Mkoa wa Songwe Isakwisa Lupembe, Mtunza Hazina wa Jimbo, ndugu Hamza Huseni na baadhi ya viongozi wa Kata na Matawi mbali mbali”.

Hali siyo shwari kule Tunduma! Hao wote waliokamatwa na wanaotafutwa kukamatwa ni viongozi wa Kisiasa ambao nyuma yao kuna kundi kubwa la watu. Ni Wagombea wa Udiwani. Hekima kubwa inahitajika katika kutatua tatizo la Tunduma. Kuna uwezekano mkubwa kuwa nyuma ya vurugu hizi kuna hujuma za kisiasa, matendo na mienendo ya baadhi ya Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi.

Pengine swali la kujiuliza ni je, baadhi ya Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi katika Mkoa wa Songwe watawajibika vipi kwa mienendo na matendo yao ambayo kwa sehemu yalipelekea vurugu zilizopelekea vifo na kutaka kusababisha Wagombea kukosa nafasi ya kuwakilisha sehemu kubwa ya watu? Hekima kubwa itumike ili kutokuwanyima haki ya kugombea Wagombea wanaowindwa kama ndege ili kukamatwa kuhusiana na vurugu za Tunduma.

Tunazidi kuonya na kutahadharisha kuhusu umuhimu wa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi, Wasimamizi wa Uchaguzi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutenda Haki ili kutunza amani ya nchi. Tunaweza kuepusha vurugu na vifo nchini kwa kutenda haki katika Uchaguzi Mkuu.

Kuonya na kutahadhalisha ni wajibu waliopewa baadhi yetu na ole wetu tusipofanya (Ezekieli 33:1-20).

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!

Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula – Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania & Afrika Mashariki