Categories
Habari

Arusha: Huku Mbunge Gambo Akidaiwa Kushawishi Wafanyabiashara Wasilipe Kodi, Yeye Asema Hatishiwi Nyau

Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amewaambia viongozi wa wilaya ya Arusha na mkurugenzi wa jiji la Arusha(DED) kuwa hatakubali kukwamishwa na viongozi wa jiji la Arusha wakati akitekeleza majukumu yake.

Gambo ameyasema hayo wakati akiongea kwenye mkutano wa Baraza la wanawake wa UWT uliofanyika kwenye hotel ya Mount Meru jiji hapa na kusisitiza kwamba hataacha kuwatetea wananchi licha ya vikwazo vingi anavyopitia kwenye mikutano yake ya kutatua kero za wananchi.

“Nimesikia kwamba wamepanga kunikamata, sitaogopa mtu Mimi ni mbunge ninayetimiza wajibu wangu sitishiwi Nyau na waache kufanya Mambo ya kishabiki” Alisema Gambo

Aliongeza kuwa Kuna mkakati unaoendeshwa na mkurugenzi wa jiji la Arusha, Dkt. John Pima wa kuwazuia watendaji kushiriki mikutano yake inayoendelea katika mitaa mbalimbali katika Jimbo la Arusha.

“Mkurugenzi amewahi kuwatoa watendaji wa halmashauri katika kikao changu lakini kwa sababu ni mgeni naamini anaendelea kujifunza atazoea” Alisema

Gambo anatuhumiwa kuwashawishi wafanyabiashara wa maduka wasilipe Kodi baada ya kuamuru maduka yaliyofungwa kwa sababu ya kutolipa Kodi yafunguliwe Jambo ambalo linaikosesha mapato serikali.