Categories
Biashara

Mitano Tena: Msako Wa Faini Za Magari Balaa, Trafiki Kila Kona

Dar es Salaam. Kama umewahi kuandikiwa faini kwa kukiuka sheria za barabarani na hujalipa imekula kwako.

Ndivyo hali ilivyo sasa kufuatia ukaguzi wa trafiki unaofanyika kila kona ya nchi, hadi katika gereji na maegesho ya magari.

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani liko katika operesheni iliyotangazwa na Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Simon Sirro la kuhakikisha wanaodaiwa wanalipa faini hizo.

Katika kuhakikisha madeni hayo yanalipwa, mbali na kuweka kamera barabarani au kusimamisha magari na kutambua gari linalodaiwa kupitia kifaa maalumu, askari wanapita katika maeneo ya maegesho ya magari na gereji ili kukusanya faini hizo.

Operesheni hiyo ilianza juzi ikiwa ni wiki mbili baada ya Mkuu wa IGP Sirro kutangaza msako huo ukilenga kukusanya zaidi ya Sh12 bilioni.

Januari 4, Sirro alisema baadhi ya wadaiwa wanaomiliki magari zaidi ya moja wamekuwa wakibandua namba za magari yasiyodaiwa na kuweka katika magari yanayodaiwa kisha kuendelea kuyatumia barabarani kwa kudhani watakuwa wamekwepa madeni yao.

ADVERTISEMENT
Mwananchi limezungumza na makamanda wa polisi wa mikoa minane nchini na kueleza mikakati mbalimbali waliyoiweka kuhakikisha wanakusanya madeni hayo, huku madereva nao wakieleza hasara ya kulimbikiza deni.

Miongoni mwa madereva waliounga mkono operesheni hiyo ni Augustine Malango, dereva wa daladala ya Masaki-Simu 2000 aliyedai kulimbikiza deni ni mtego wa kuingiza hasara kwa dereva anayejitambua.

“Ukikaa na deni trafiki wakajua kesho utampoza Sh5000, mwingine Sh3000 halafu wakati huo deni la kosa moja Sh30,000 linazidi kuzaa, ukipiga hesabu utaona ni bora ulipe,” alisema Malango.

Kulingana na taratibu za kulipa deni hilo, unapoandikiwa Sh30,000 unatakiwa ukilipe ndani ya siku saba na kama usipofanya hivyo deni hilo huongezeka kwa Sh7,500 kila wiki kukomea Sh60,000 kwa kosa moja.

Hamza Lyeme alisema operesheni hiyo itaongeza umakini wa madereva barabarani na kupunguza ajali za makosa ya kibinadamu.

“Pamoja na vikwazo vingine vya maofisa wa usalama barabarani lakini madereva wengi wamekuwa wakorofi. Hamna namna dawa ya deni kulipa,” alisema Lyeme.

Kuanzia juzi, baadhi ya maofisa wa polisi katika mikoa hiyo wakiongozana na baadhi ya maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wameendelea na ukaguzi wa magari mitaani, maeneo ya kuegesha magari, gereji, au maeneo mahali penye mzunguko wa magari.

Licha ya kutokuwa na takwimu za ukamataji ndani ya siku mbili zilizopita, makamanda wa mikoa tisa waliozungumza na gazeti hili jana walisema ukaguzi huo utafanyika kwa magari yaliyopo ndani ya mkoa husika na yale yanayopita kuelekea mikoa myingine.

“Tumeanza jana (juzi) tunapita mitaani, mwitikio wa malipo ni mzuri. Japo sina takwimu lakini tunatakiwa kushughulikia deni la mkoa wetu ambalo ni sehemu ya deni la zaidi ya Sh12 bilioni, tunasisitiza wajitokeze kulipa madeni yao,” alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, James Manyama.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei alisema wanatakiwa kuhakikisha wanakusanya Sh333 milioni kupitia operesheni hiyo huku Wankyo Nyigesa, RPC wa Pwani, akisisitiza madereva wanaodaiwa kujisalimisha ndani ya mkoa huo.

Oparesheni hiyo pia inaendelea chini ya RPC, Gilles Muroto kama ilivyo kwa Hamis Issa, RPC wa Njombe aliyesema tayari amekamata zaidi ya magari 60 juzi, na wote walilipa madeni yao.

Kwa upande wale Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Richard Abwao alisema oparesheni hiyo inaanza rasmi leo kwa msako utakaokuwa wa kushtukiza katika eneo lolote bila kuweka wazi.

“Lengo ni kukusanya madeni hayo, tunasisitiza wenye madeni walipe ili waendelee kuwa na amani,” alisema Abwao.

“Muda wa kulipa deni ni ndani ya siku saba, kwa hiyo tukikamata mwenye deni anatakiwa kulipa vinginevyo hatua za kisheria zinachukuliwa, kwa sababu alishindwa kulipa ndani ya muda husika,” alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Henry Mwaibambe.

Hata hivyo, Mwaibambe alisema hatua hiyo haitaathiri usafirishaji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Simon Maigwa alisema tayari Sh17.2 milioni zilikusanywa juzi katika magari 87 yaliyokamatwa kupitia operesheni hiyo.

Chanzo: Mwananchi