Categories
Biashara

Macho Yote Kwa Membe Baada Ya ACT – Wazalendo Kutamka Itatangaza Mgombea Urais Inayemuunga Mkono (Ikimaanisha Si “Mgombea Wao” Membe)

Tamko hilo la Zitto ni kama kupigia mstari kauli hii ya Maalim Seif Sharif Hamad

Macho na masikio sasa yaelekezwa kwa Bernard Membe, kada wa zamani wa CCM aliyefukuzwa na chama hicho tawala kisha akajiunga na ACT-Wazalendo, kabla ya kupitishwa kuwa mgombea wa chama hicho katika nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Macho na masikio yanaelekezwa kwake kwa sababu mara baada ya kauli ya Maalim Seif, Membe aliweka msimamo wake bayana kuwa yeye ndiye mgombea wa nafasi ya urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo. Je atakubali kuachia nafasi hiyo?

Pengine kasoro ya kiufundi inayofanywa na ACT-Wazalendo ni kwenye mawasiliano. Kauli ya Maalim Seif haikutolewa rasmi na yeye mwenyewe bali kada mmoja wa chama hicho, “Ndolezi,” aliyetwiti, tena kwa Kiingereza, pengine ili watu wasiomudu lugha hiyo wasielewe kilichosemwa.

Na tangu wakati huo chama hicho ambacho kimekuwa makini katika utendaji kazi wake hakijatamka lolote kuhusu kauli ya Maalim Seif wala hiyo ya Membe.

Hata hivyo, ni wazi kuwa endapo chama hicho kitatoa matamko yanayokinzana na “mgombea wake” Membe kitakuwa kama kinahujumu kampeni za “mgombea halisi wa upinzani,” Tundu Lissu, anayegombea nafasi ya urais kwa tiketi ya Chadema.

Kwa upande mwingine, “sintofahamu” hii kuhusu Membe ni funzo jingine chungu kwa vyama vya upinzani katika “tamaa” yao ya kupokea “makapi” ya CCM. Vyama hivi vinapaswa kufahamu kuwa kama chama chenye kila kasoro kama CCM kinadiriki kumkataa mwanasiasa wake, kwanini “makapi” hayo yawe lulu kwa hao wapinzani wanaotarajiwa kuwa bora zaidi ya CCM?

Ilidhaniwa kuwa “jinsi Lowassa alivyoiingiza mkenge Chadema” ingetosha kuitahadharisha kuhusu Membe, ambaye baadhi ya watu wanadhani kuwa “amepandikizwa tu kwa minajili ya kubomoa upinzani,” hasa ikizingatiwa kuwa huko nyuma alikuwa mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa.