Categories
Biashara

CHADEMA Yakanusha Alichosema Halima Mdee na Wenzie 18. Yasisitiza Uamuzi Wa Kuwavua Uanachama Unapaswa Kuzingatiwa Na Mamlaka

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA)

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KAULI YA WALIOKUWA WANACHAMA 19

Tumesikia kauli iliyotolewa na waliokuwa Wanachama wetu 19 waliochukuliwa hatua na Kamati Kuu ya kufukuzwa uanachama kuwa wanakusudia kukata rufaa kwa mujibu wa Katiba ya Chama toleo la Desemba, 2019.

Napenda kutoa ufafanuzi kwenye baadhi ya hoja kama ifuatavyo;

1. Kuwa Kuna baadhi ya Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati Kuu ambao walikuwa wanahamasisha Wanachama ili wawafanyie fujo waliokuwa Wanachama 19, napenda kueleza kwamba Chama hakijawahi kuletewa malalamiko yoyote wala ushahidi na waliokuwa wanachama 19 kabla ya kikao hicho kuwa kuna wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama waliokuwa wakihamasisha kwamba wakifika Makao Makuu wafanyiwe fujo.

Aidha, walipoandika barua kuhusu hofu ya usalama wao, Chama kiliwaelekeza kwamba badala ya kufika Makao Makuu ya Chama kama ilivyokuwa imeelekezwa awali wafike katika Hotel ya Ledger Plaza Bahari Beach ili wawe huru kufika na kujielekeza mbele ya kikao cha Kamati Kuu.

Kwa maana hiyo suala hilo limetumika tu kama kisingizio dhidi ya uamuzi wao wa kukwepa kuja kujitetea mbele ya kikao cha Kamati Kuu.

2. Kuhusu suala la kuomba kuongezewa muda, walifahamishwa kwa barua kuwa waje mbele ya Kamati Kuu na wawasilishe maombi yao ya kuongeza muda ili Kamati Kuu itafakari na kuona kama inaweza kuwaongezea muda. Badala ya kufanya hivyo waliamua kwa makusudi kukaidi kufanya hivyo.

Aidha, ifahamike kuwa Kamati Kuu ina mamlaka kwa mujibu wa Kanuni za Chama ibara ya 6.5.1(d) kuchukua hatua za dharura bila kufungwa na masharti ya siku 14 isipokua anayelalamikiwa atakua na haki ya kuitwa kwenye kikao.

3. Kwamba pamoja na nia yao ya kukata rufaa, mpaka sasa Chama hakijapokea rufaa yoyote na kwamba izingatiwe uamuzi wa kuwavua nafasi zao za uongozi ndani ya chama na kuwafukuza uanachama utaendelea kutamalaki na unapaswa kuzingatiwa na wanachama wote na mamlaka zote hadi hapo utakapobatilishwa na Baraza Kuu iwapo wahusika wakikata rufaa na rufaa yao kukubaliwa.

John Mrema -Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje.